Ushahidi wa Askofu Chilongani kesi ya Sepeku

Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi Central Tanganyika (Dodoma), Dk Dickson Chilongani (59) ameieleza mahakama kuwa alijihisi furaha na huzuni, Askofu mkuu wa kwanza wa kanisa hilo, hayati John Sepeku alipozawadiwa shamba na nyumba.

Dk Chilongani ameieleza hayo Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi leo Agosti 29, 2025, alipotoa ushahidi katika kesi ya ardhi iliyofunguliwa na Bernardo Sepeku.

Bila kufafanua sababu za yeye kujihisi furaha na huzuni, Askofu Chilongani ambaye ni shahidi wa nne wa upande wa utetezi, ametoa maelezo hayo alipohojiwa na jopo la mawakili wa mlalamikaji katika kesi hiyo, wakiongozwa na Deogratias Butawantemi. Wengine ni Gwamaka Sekela na Eric Amon.

Dk Chilongani aliyekuwa Katibu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania mwaka 2010 hadi 2013, ametoa ushahidi mbele ya Jaji Arafa Msafiri.

Bernardo ambaye ni mtoto wa hayati John Sepeku, amefungua kesi ya madai akipinga kunyang’anywa zawadi ya kiwanja alichopewa baba yake mwaka 1978 na kanisa hilo.

Kesi hiyo ya ardhi namba 378/2023 imefunguliwa dhidi ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa Angilana Tanzania, Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam na Kampuni ya Xinrong Plastic Waste Industry Co Ltd.

Katika madai yake, anaomba alipwe Sh3.72 bilioni zikiwa ni fidia ya hasara ya kifedha iliyopatikana kutokana na uvamizi wa ardhi katika kiwanja hicho.

Katika ushahidi wa msingi akiongozwa na Wakili Denis Malamba, Dk Chilongani amesema kikao cha Sinodi kina nguvu katika imani na utawala, lakini hakina nguvu katika masuala ya kutoa mali au zawadi.

Amedai hata utaratibu uliotumika kumpa zawadi Askofu Sepuku haukufuata sheria na taratibu kwa kuwa Bodi ya Wadhamini wa kanisa hilo haikuwa na kikao cha kuidhinisha zawadi hiyo.

“Shamba la Buza na nyumba iliyopo Buguruni ambavyo vilitolewa kama zawadi kwa Askofu Sepeku, vipo chini ya Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania,” amedai shahidi.

Amedai ili mali itolewa na bodi ya wadhamini ni lazima wakae kikao kwanza.

Dk Chilongani amedai bodi ya wadhamini ina uwezo wa kupinga uamuzi uliofanywa na kikao cha Sinodi, huku Sinodi nayo ina uwezo wa kupinga uamuzi uliotolewa na Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Anglikana Tanzania.

Amedai mgogoro huo wa ardhi baina ya Bernardo Sepetu dhidi ya wadhamini wa bodi hiyo, ameufahamu miaka minne iliyopita baada ya kufunguliwa kesi mahakamani.

Katika ushahidi wa upande wa madai uliotolewa na mashahidi mbalimbali wakiwamo wajumbe wa bodi ya wadhamini na maaskofu wengine wa kanisa hilo, akiwemo Askofu Oscar Mnung’a, amedai Askofu Sepeku alipewa zaidi hiyo na Dayosisi ya Dar es Salaam mwaka 1980.

Pendekezo la kumzawadia Askofu Sepeku shamba na nyumba lilitolewa awali na Kamati ya Kudumu ya Kanisa hilo, Dayosisi ya Dar es Salaam katika kikao cha Desemba 8, 1978.

‎‎Sinodi ya Dayosisi hiyo katika kikao cha Machi 8 na 9, 1980 iliridhia na kuazimia kumpatia Askofu Sepeku zawadi ya ardhi, shamba la eka 20 lililoko Buza, wilayani Temeke na nyumba eneo la Kichwere, Buguruni, wilayani Ilala, Dar es Salaam.

Hata hivyo, Askofu Chilongani amekatana kutambua shamba na nyumba hiyo kutolewa kwa Askofu Sepeku kama zawadi kwa madai kuwa, zawadi hiyo haikufuata sheria na kanuni, japokuwa amekiri katiba ya mwaka 1970 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2004, sura ya 10 inaeleza mamlaka ya wadhamini wa bodi ya kanisa hilo ni kutunza mali za dayosisi.

Akihojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa wadai, Butawantemi, Sekela na Amon, amedai bodi ya wadhamini ndiyo ina mamlaka ya kutoa zawadi na siyo kanisa wala mkutano wa Sinodi ambao una mamlaka ya juu ya kutoa zawadi.

Alipoulizwa amefika mahakamani kufanya nini? Amedai amefika kutoa ushahidi kwa niaba ya Bodi ya Wadhamni wa Kanisa la Anglikana Tanzania kwa sababu yeye ni mjumbe wa bodi hiyo.

Amedai wajumbe wa bodi hiyo wapo 28 nchi nzima na wote ni maaskofu.

Jaji Msafiri ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 12, 2025 siku ambayo Askofu Jackson Sostenes wa Dayosisi ya Dar es Salaam atatoa ushahidi katika kesi hiyo.