Utekelezaji amri ya Waitara kumfidia Maswi Sh6 bilioni wasimamishwa

Arusha. Mahakama ya Rufaa imesimamisha utekelezwaji wa uamuzi na amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, iliyomuamuru aliyekuwa mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara na wenzake kumlipa fidia ya Sh6 bilioni, Eliakim Maswi, ambaye kwa sasa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria.

Mahakama imesitisha uamuzi na amri zilizotolewa Juni 16, 2025 katika kesi ya madai namba 23/2023, kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa rufaa ambayo Waitara anakisudia kukata kupinga uamuzi na amri ya Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Mahakama ya Rufaa imetoa sharti kwa Waitara kuweka kwa Msajili wa Mahakama dhamana ya benki isiyoweza kubatilishwa ya Sh3 bilioni ndani ya siku 60 tangu ulipotolewa uamuzi huo.

Uamuzi wa Mahakama ya Rufaa unaopatikana kwenye tovuti ya Mahakama umetolewa Agosti 26, 2025 na Jaji Agness Mgeyekwa, kutokana na maombi ya Waitara katika shauri la maombi ya kusimamisha utekelezaji wa uamuzi na amri ya Mahakama Kuu.

Waitara alifungua shauri hilo dhidi ya Maswi akiiomba Mahakama ya Rufaa kusimamisha utekelezaji wa uamuzi na amri ya Mahakama Kuu, kusubiri uamuzi wa rufaa anayokusudia kuikata.

Jaji Mgeyekwa amesema baada ya kupitia hoja za pande zote mbili, amekubali maombi hayo na kusitisha uamuzi wa Mahakama Kuu hadi rufaa itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Wakili Hekima Mwasipu, aliyemwakilisha Waitara, wakati wa usikilizwaji wa maombi alieleza Mahakama kuwa mteja wake amekidhi vigezo vya kupata amri ya kusimamishwa utekelezaji wa uamuzi unaokusudiwa kukatiwa rufaa, ikiwa ni pamoja na kufunguliwa ndani ya muda unaoelezwa katika kanuni.

Alidai endapo utekelezaji utafanyika, mwombaji atapata hasara kubwa akirejea hati ya kiapo kuwa, nyumba iliyotajwa ndiyo anayoishi pamoja na familia yake.

Aliiomba Mahakama maombi hayo yakubaliwe bila gharama, akiomba kupewa siku 90 ili kuweka zuio.

Kwa upande wake, Wakili Kassimu Gilla, anayemwakilisha Maswi alipinga maombi hayo akidai mwombaji ameshindwa kukidhi matakwa ya kanuni ili kupewa amri ya kusimamisha utekelezaji wa hukumu.

Amedai maombi kuwa Waitara atapata hasara kubwa hayana uthibitisho, hivyo aliiomba Mahakama itupilie mbali maombi hayo, akieleza hayana mashiko. Pia aliomba kila upande ubebe gharama zake.

Alisema mali inayozungumza kwenye hati ya kiapo ni nyumba ya makazi, hivyo kuashiria ni mali ya ndoa, aliiomba Mahakama kuzingatia dhamana ya benki ya Sh3 bilioni.

Jaji Mgeyekwa baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili amesema hakuna ubishi kwamba mwombaji amezingatia matakwa chini ya kanuni na maombi yamewasilishwa ndani ya muda uliowekwa.

Amesema ingawa hati ya kiapo haielezi kwa uwazi kama nyumba inayohusika katika utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu ni mali ya ndoa, kauli yake kwamba anaishi humo na familia yake, inatosha kuwa ni nyumba ya familia.

“Nimeridhika kwamba huu ni msingi sahihi wa kukisia kuwa hasara kubwa ingetokea ikiwa utekelezaji ungeendelea,” amesema.

Jaji amesema katika aya ya 13 ya hati ya kiapo, mwombaji anaonyesha nia ya kutoa dhamana ya benki, ingawa wakili wa mjibu maombi aliibua wasiwasi kuhusu muda uliopendekezwa wa siku 90, lakini anaona kiasi kinachohusika ni kikubwa.

Amesema katika mazingira hayo na kwa masilahi ya haki, mwombaji anapaswa kupewa muda wa kutosha.

“Kwa hiyo, ninayakubali maombi haya na ninaamuru kusimamishwa kwa amri ya Juni 16, 2025 kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa rufaa iliyokusudiwa, ” amesema.

Pia, kwa mujibu wa kanuni, ameamuru mwombaji kuweka kwa Msajili wa Mahakama dhamana ya benki isiyoweza kubatilishwa ya Sh3 bilioni, ambayo inapaswa kuwekwa ndani ya siku 60 kuanzia tarehe ya kutolewa kwa uamuzi huo.

Juni 16, 2025 Mahakama Kuu Kanda ya Musoma ilimuamuru Waitara na wenzake wawili kumlipa fidia ya Sh6 bilioni, Maswi baada ya kupatikana na hatia katika kesi ya kashfa iliyokuwa ikiwakabili.

Hukumu ilitolewa na Jaji Marlin Komba aliyesema kwa mujibu wa ushahidi uliowasilisha mahakamani, alijiridhisha pasipo shaka kuwa wadaiwa walitenda kosa hilo kinyume cha sheria.

Jaji Komba aliwahukumu wadaiwa kumlipa Maswi Sh1 bilioni kama fidia ya adhabu ya udhalilishaji baada ya kubainika kuwa walitumia maneno ya uongo na kumkashifu.

Vilevile, aliamuru Maswi alipwe Sh5 bilioni kama fidia ya madhara ya jumla na pia kuombwa radhi hadharani kupitia vyombo vya habari.

Alisema kabla ya hukumu wadaiwa walitakiwa kuomba msamaha, lakini walikataa kufanya hivyo.

Jaji alisema maneno ya Waitara hayakuwa kashfa kwa Maswi pekee bali kwa watumishi wa umma kwa ujumla na akuwa aliamua kufanya hivyo kwa sababu hajawahi kuwa mtumishi wa umma.

Katika kesi hiyo, Maswi alidai Agosti 9, 2023, Waitara alitoa maneno ya kashfa dhidi yake katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kijiji cha Mtana, Kata ya Manga, wilayani Tarime mkoani Mara, uliohudhuriwa na watu zaidi ya 500.

Alidai maneno hayo yaliandikwa na kuonyeshwa kupitia televisheni ya mtandaoni ya Mara TV na yalikuwa ya uongo, yenye nia ovu na yalilenga kushusha hadhi yake.

Walalamikiwa wengine walikuwa Karoli Jacob na Mara TV. Alidai kwenye mkutano huo, Waitara alisema Maswi anahusika na kuwajibika na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya nafasi yake kwenye utumishi wa umma, kama Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Ununuzi wa Umma (PPRA).

Maswa alidai televisheni ya mtandaoni ya Mara TV ilichapisha maneno hayo na hadi Agosti 23, 2023 chapisho hilo lilitazamwa na watu zaidi ya 280 kutoka duniani kote.