Wadau wa nishati kukutana kujadili fursa na changamoto sekta ya gesi asilia

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk James Mataragio amesema Serikali impenga kuwakutanisha wadau mbalimbali wa gesi asilia (CNG) na gesi ya mitungi (LPG) kujadili fursa na namna ya kutanzua changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.

Wadau hao watakutana baada ya uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu, jambo ambalo linatajwa kuwa suluhu kwa wawekezaji hao kupunguza gharama za uwekezaji na kuondoa vihatarishi kwenye biashara ya gesi.

Dk Mataragio ametoa kauli hiyo leo Agosti 29, 2025katika ziara iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutembelea vituo vya kujaza gesi asilia kwenye magari yanayojengwa maeneo ya Mikocheni, Mbezi Afrikana, Tegeta na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

”Teknolojia inakuwa kwa haraka sana, zipo kampuni zinakuja na teknolojia mpya kwenye sekta ya gesi na zinatofautiana, wapo wanaoagiza vifaa vyao China, wengine Canada,

Tukiwakutanisha pamoja watabadilishana uzoefu na hiyo itasaidia kupunguza gharama za uwekezaji, mkutano huu utafanyika baada ya uchaguzi mkuu mwaka huu,”amesema.

Naibu Katibu Mkuu huyo, amesema kumekuwa na dhana ya baadhi ya wawekezaji kudai kuwekeza sekta ya gesi kuna hatari kubwa na gharama za uwekezaji ni kubwa lakini uhalisia ni tofauti.

“Gharama ya uwekezaji inategemea unawekeza kwenye kituo cha ukubwa gani, mfano kituo cha Tanhealh hicho kimejengwa kwa Sh1 bilioni, sisi tunawaomba kama Serikali wawekezaji waendelee kuwekeza tasisi za Serikali zimejipanga kuwahudumia kwa haraka,”amesema

Pia, Dk Mataragio amesema kumekuwa na changamoto kwa benki kutoa mikopo kwa wawekezaji katika sekta ya gesi asilia.

“Mwanzoni ilikuwa ngumu kwa benki zetu kutoa mikopo kwa wekezaji kutokana na kutofahamu hatari za biashara husika, sasa baadhi zimeanza kuelewa biashara ikoje na imeanza kutoa mikopo. Nitoe rai kwa mabenki wafahamu tu biashara hii ni kama zilivyo zingine, wasisite kutoa mikopo kwa wawekezaji katika sekta hii,”amesema.

Amesema kwa sasa dhamira ya Serikali na sekta binafsi ni kuhakikisha gesi asilia inasambaa kwa kasi ili kufikia 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi.

Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya BQ Construction Limited Profesa John Bura amesema wanaanzisha kituo cha gesi mama ambacho kitakuwa na uwezo wa kujaza magari 180 kwa siku kwa kutumia pampu tatu akidokeza changamoto wanayokumbana nayo.

“Mradi huu utakamilika baada ya miezi sita na tutatumia Sh5 bilioni, changamoto kubwa kwenye sekta hii ni mikopo kutoka benki, hawatoai kutokana na kile wanachodai hawajui hasara zinazopatikana kwenye miradi ya namna hii, lakini kama sisi wawekezaji tuna utayari wa kuwekeza,”amesema.

Kwa upande wake Meneja mradi wa gesi asilia, kituo cha gesia kwenye magari Puma Chagaka Kalimbia amesema wanajenga kituo mama cha kujaza gesi kwenye magari kwa Sh6 bilioni

“Kituo kitakamilika Oktoba mwaka huu, kitakuwa na pampu nne zenye uwezo wa kujaza gesi kwenye magari nane kwa wakati mmoja, tulikuwa tujenge na kituo cha kubadili mifumo ya gari kutumia gesi ila tumeona sasa magari yanaingia nchini yakiwa yamebadilishwa,

Tunaishukuru Serikali zipo tozo zimeondolewa kwenye sekta hii imetusaidia kukuza sekta,”amesema.