Wafanyabishara nchi sita jirani kunufaika fursa kiuchumi Bandari ya Tanga

Bandari ya Tanga imepanua wigo wa kibiashara kutokana na uboreshaji wa miundombinu uliofanyika na kuifanya kuwa lango kuu la kibiashara na uwezo wa kuhudumia wateja kutoka nchi jirani.

Miongoni mwa nchi ambazo zitanufaika na bandari hiyo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi, Uganda, Zambia, Malawi na Zimbabwe.

Sababu ya bandari hiyo kuwa lango la kibiashara ni kutokana na maboresho yaliyofanyika kwenye miundombinu na huduma kwa wateja, hatua iliyoongeza ufanisi na kupunguza gharama za usafirishaji.

Meneja wa Bandari ya Tanga, Masoud Mrisha amesema maboresho hayo yameifanya bandari hiyo kujipambanua kama kituo salama, chenye ufanisi mkubwa na nafuu kwa wateja wa sekta ya usafirishaji.

“Bandari ya Tanga sasa ina uwezo mkubwa wa kuhudumia meli kubwa zaidi kwa haraka, jambo ambalo limepunguza muda wa meli kukaa bandarini hadi siku tatu pekee. Hii imeongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kuelekea nchi jirani,” amesema Mrisha.

Maboresho hayo yamekuwa chachu ya kuimarisha nafasi ya bandari hiyo katika ushindani wa kikanda, huku wadau wakipongeza jitihada za Serikali katika kubadilisha sura ya bandari hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi Kolimba, ametoa rai kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia Bandari ya Tanga.

“Uwekezaji mkubwa uliofanyika ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya kuhakikisha bandari hii inakuwa chachu ya uchumi wa Taifa na njia rahisi kwa wafanyabiashara wetu,” amesema Kolimba.