Mbeya. Watu wawili wakazi wa Mkoa wa Mbeya na Morogoro wamehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja akiwepo Mwanamke Tecla Lumala (24) baada ya kupatikana na makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi.
Hukumu hizo zimesomwa kwa nyakati tofauti katika mahakama ya Wilaya ya Mbeya na Rungwe kwa kipindi cha mwezi Agosti 18 mpaka 20 mwaka huu.
Awali, Mahakama ya Wilaya ya Rungwe Mkoa wa Mbeya, imemhukumu miaka 30 jela mwanamke Tecla Lumala (24) Mkazi wa Mkoa wa Morogoro kwa tuhuma za kupatikana na kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilogramu 6.8.
Hukumu hiyo imesomwa Agosti 18, 2025 mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Rungwe, Mwinjuma Bwanga baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa jamhuri.
Imeelezwa kuwa Desemba 22, 2024 katika kizuizi cha Kayuki kilichopo Kijiji cha Ngujubwaje, Kata ya Ilima, Wilaya ya Rungwe mshtakiwa alikamatwa akisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilogramu 6.8.
Kufuastia ushahidi ulio wasilishwa na upande wa Jamhuri mshtakiwa alitiwa hatiani na hakimu Bwanga kusoma hukumu ya kutumikia kifungo cha miaka 30 jela ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kusafirisha dawa za kulevya wakati wakitambua ni kosa kisheria.
Katika hatua nyingine Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela Frank Muhagama (28) Mkazi wa Isanga jijini hapa baada ya kupatikana na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.
Hukumu hiyo ilisomwa Agosti 20, 2025 mbele ya Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Mbeya, Paul Ntumo, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo pasipo shaka.
Imeelezwa mshtakiwa alitenda kosa la kumvamia na kumshambulia Nadhir Thawaer mmiliki wa Shule ya Msingi Reverside iliyopo eneo la Sokoine jijini hapa na kisha kumpora Sh3 milioni na mkufu wa dhahabu wenye thamani ya Sh6 milioni.
Mshtakiwa alitenda kosa hilo Machi 18,2025, majira ya saa 9.00 usiku huko eneo Riverside Sokoine jijini hapa ambapo baada ya kufikishwa mahakamani alikiri kutenda kosa hilo na hivyo kutiwa hatiani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema hukumu hizo ni sehemu ya mafanikio ya kesi zilizo funguliwa na kufishwa mahakamani na Jeshi la Polisi.
Kuzaga amesema kwa kipindi cha mwezi Agosti pekee jumla ya kesi 170 zilifikishwa mahakama kati ya hizo 62 zilipata mafanikio washtakiwa wametiwa hatiani na kuhukumiwa vifungo tofauti na 108 zinaendelea kwa hatua mbalimbali.
Katika hatua nyingine Kamanda Kuzaga ameonya jamii kujiepusha na matukio ya kihalifu na unyang’anyi kwani Polisi hawajalala watakamatwa na kufikishwa mahakamani.