Dar es Salaam. Wakati uongozi wa tawi la ACT-Wazalendo la Mafifi mkoani Iringa, ukitangaza kumfuta uanachama kada wake Monalisa Ndala, yeye ameibuka akipinga hatua hiyo.
Monalisa amepinga hatua hiyo akibainisha kuwa yeye bado ni mwanachama hai wa ACT-Wazalendo tawi la Kibangu, wilayani Ubungo, mkoani Dar es Salaam na siyo Mafifi kama ilivyoainishwa katika barua ya kufutwa uanachama wake.
Katika kikao cha kamati ya uongozi wa tawi la Mafifi kilichofanyika Agosti 28, 2025, Kata ya Kihesa mkoani Iringa inaelezwa kiliazimia kumvua uanachama Monalisa kwa madai ya kushindwa kutekeleza matakwa ya katiba ya chama hicho, hivyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa mwanachama.
“Uamuzi huu umetolewa kwa mujibu wa katiba ya ACT-Wazalendo ya mwaka 2015, Toleo la 2024, hususani Ibara ya 8 (2) (a) (b), (d),” alisema Neema Kivamba, katibu wa tawi hilo katika barua aliyoitoa jana Agosti 29.
Kivamba alisema kwa mujibu wa Ibara ya 97 (1) (d), kamati ilijiridhisha kuwa Monalisa ameshindwa kutekeleza matakwa ya katiba ya chama hicho, hivyo kupoteza sifa za kuendelea kuwa mwanachama.
Leo Jumamosi Agosti 30, 2025 Monalisa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam amesema: “Mimi ni mwanachama hai wa ACT-Wazalendo, ni kiongozi na katibu mwenezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, kadi yangu inasomeka Dar es Salaam, ni mwenyekiti wa Jimbo la Kibamba, sasa sijui Mafifi inatoka wapi?”
Monalisa ameeleza mwaka 2024 katika uchaguzi wa ndani, ACT-Wazalendo kiliwekwa mfumo wa kikanda unaotaka ili kada awe mjumbe wa kamati kuu au halmashauri kuu lazima awanie kutokea kanda.
Amesema yeye aliwania ujumbe wa halmashauri kuu katika kanda ya nyanda za juu kusini, ndiyo maana katika barua ya kufutwa uanachama wametumia Mkoa wa Iringa.
Baada ya uchaguzi huo kuisha na kuibuka kidedea, Monalisa alisema aliitwa na mwanasheria mkuu wa chama hicho akaelezwa alikiuka taratibu na kanuni za chama hicho za kuwania uongozi wakati yeye ni mwenezi wa Dar es Salaam na nafasi yake ikatenguliwa kutokana na kukiuka taratibu.
“Sijapoteza sifa za kuwa mwanachama wa ACT-Wazalendo, nitaupigania uanachama wangu kwa nguvu zote. Mimi bado mwanachama ACT-Wazalendo wa Dar es Salaam siyo Iringa. Juzi nilialikwa kwenye kikao cha uongozi wa Dar es Salaam, sasa nawezaje kuwa mwanachama wa maeneo mawili?” amehoji.
Kutokana na hilo, Monalisa ameipa siku mbili ofisi ya Katibu Mkuu (Ado Shaibu) kuikana barua hiyo, akidai inakidhalilisha chama hicho na imekuwa ikisambazwa na wasaidizi wa mtendaji mkuu wa ACT-Wazalendo.
“Mimi Monalisa Joseph Ndala ni mwanachama hai wa ACT-Wazalendo na uthibitisho wangu ni kadi yangu ya uanachama, Mafifi siyo tawi langu, sijawahi kuitwa. Sitavumilia kitendo hiki, nitaendelea kuupigania uanachama wangu kwa jasho na damu,” amesema.
Endapo mambo yakienda tofauti, amesema atakwenda mahakamani kudai haki, lakini kwa hatua ya sasa hawezi kufika huko kwa sababu yeye ni mwanachama halali wa chama hicho tawi Kibangu, Dar es Salaam.
“Katibu mkuu ajitenge na suala hili lililofanywa na wasaidizi, yeye ndiye wa kukinusuru chama, wakikaidi wasinilaumu. Nilichokifanya ni kutimizi wajibu wangu, sikufanya makosa yoyote,” amesema.
Alipotafutwa na Mwananchi, Ado alielekeza atafutwe Shangwe Ayo (Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma, ACT-Wazalendo).
Shangwe amesema hakuna watakachokifanya kwa maelekezo ya Monalisa.
“Hatufanyi lolote aliloelekeza Monalisa, kwani yeye ni nani? Monalisa alihamisha uanachama wake mwaka 2024 kuelekea nyanda za juu kusini ili kushinda ujumbe wa halmashauri kuu ya chama. Alihamisha uanachama kutoka Ubungo kwenda Iringa,” amesema na kuongeza:
“Baada ya kuhamisha uanachama na kushinda ujumbe wa halmashauri kuu aliwekewa pingamizi na kamati ilipoketi ilijiridhisha kuwa Monalisa alikiuka taratibu na kumvua ujumbe wa halmashauri kuu,”amesema.
Amesema baada ya mchakato huo Monalisa hakuwahi kurudi katika chama kutaka kuurejesha uanachama wake Ubungo kutoka Iringa.
“Hizo siku mbili alizozitoa hatuna muda wa kumjibu, hatumuogopi na tuna uthibitisho wa kumuonyesha kadi yake ya mwisho alisajiliwa wapi,” amesema.
Hatua ya kufutwa uanachama wa Monalisa, imechukuliwa siku chache tangu alipowasilisha malalamiko kupinga uteuzi wa Luhaga Mpina kuwa mtiania wa urais wa chama hicho Agosti 19, 2025.
Pingamizi hilo, Monalisa aliwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na hatimaye Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) ikamuengua kuwania urais kupitia chama hicho.
Sababu kuu iliyoelezwa na Monalisa ni kwamba, Mpina alipata uanachama Agosti 5, 2025, nje ya muda wa kisheria wa kuchukua fomu za kugombea ndani ya chama, ambapo ilipaswa kuwa kabla ya Mei 25, 2025.