Chan 2024: Morocco v Madagascar Fainali ya kibabe

MASHINDANO ya (CHAN) PAMOJA 2024 yanafikia kilele chake leo Jumamosi, jijini Nairobi, Kenya wakati mabingwa mara mbili wa michuano hiyo, Morocco watakapovaana na Madagascar kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi Kasarani, baada ya jana Ijumaa kushuhudia mechi ya mshindi wa tatu ikipigwa jijini Kampala, Uganda kati ya Sudan dhidi ya Senegal.

Fainali hii ya nane ya CHAN tangu kuanzishwa mwaka 2009 inazikutanisha timu mbili zenye historia tofauti. Madagascar ni mara ya kwanza kufika hatua hiyo, huku kwa Morocco ikiwania kutwaa taji la tatu na kuwa nchi iliyobeba mara nyingi zaidi kwani ni wao na DR Congo iliyong’olewa hatua ya makundi ikiwa Kundi A ndizo zimetwaa mara nyingi, mbili kila moja.

Hii ni fainali ya tatu kwa Morocco na rekodi zinaonyesha katika fainali mbili ilizocheza haijapoteza.

Madagascar imekuwa taifa la 13 tofauti kufika hatua ya fainali na ushindi kwao utawafanya kuwa timu ya kwanza kutoka Kusini mwa Afrika kutwaa taji hilo.

Aidha wao ndio taifa la kwanza kutoka visiwani kufika hatua ya fainali ya CHAN, jambo linaloongeza upekee wa safari yao, ikumbukwe kuwa Madagascar ilishika nafasi ya pili Kundi B ambalo liliongozwa na Taifa Stars iliyoishia robo baada ya kutolewa na Morocco.

Kwa upande wa Morocco, inatafuta kuweka rekodi mpya ya kuwa timu ya kwanza kushinda mara tatu. Tayari wameshinda kwa kishindo fainali mbili, ikiifunga Nigeria 4-0 mwaka 2018 na Mali 2-0 mwaka 2020.

Hii inawapa heshima lakini presha ya kuthibitisha ubora wao mbele ya Madagascar yenye kiu ya mafanikio.

Madagascar ilifika fainali baada ya ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Sudan katika nusu fainali. Safu yao ya ushambuliaji imeonyesha uhai mkubwa kwa kufunga katika michezo mitano mfululizo.

Nyota kama Toky Rakotondraibe, aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Sudan na Lalaina Rafanomezantsoa, mwenye pasi tatu za mabao, wamekuwa uti wa mgongo wa timu hiyo.

Safu ya ulinzi ya Madagascar pia imejidhihirisha kwa uimara. Kipa Michel Ramandimbisoa amekuwa shujaa wao akiwa na ‘clean sheets’ tatu na kuokoa mashuti 25, kiwango kikubwa zaidi miongoni mwa makipa wote.

Kwa Morocco, safari yao ya fainali haikuwa rahisi. Walipambana na Senegal na kufuzu kupitia penalti. Hata hivyo, uzoefu mkubwa katika hatua za mtoano unawapa faida, kwani wamecheza michezo tisa ya mtoano wakishinda minane.

Madagascar imepoteza mechi moja pekee ilizocheza katika CHAN hii mbele ya Tanzania katika hatua ya makundi. Tangu hapo, imeonekana kujipanga upya na kuonyesha  kiwango bora hadi kufika fainali, hali inayoongeza matumaini ya kufanya makubwa katika fainali ya leo.

Kwa upande wa Morocco, imepoteza mechi moja pekee katika michezo 19 ya CHAN iliyocheza tangu kushiriki kwao kwa mara ya kwanza (W15 D3). Takwimu hizi zinawafanya kuonekana kama timu yenye nafasi kubwa, lakini inaongeza changamoto kwa Madagascar kuvunja mwiko huo.

Takwimu zinaonyesha kuwa tangu mwaka 2011, angalau timu moja iliyofika fainali ya CHAN haijawahi kushinda taji hilo hapo awali. Ikiwa Madagascar itafanikiwa, itakuwa mabingwa wapya wa pili mfululizo baada ya Senegal kushinda mwaka 2022.

CHA 01

Moja ya nyota wakubwa wa Morocco ni mshambuliaji hatari, Oussama Lamlioui anayongoza orodha ya wafungaji hadi sasa akiwa na mabao manne na aliyeibuka mchezaji bora wa mechi mara moja ambapo ni dhidi ya DR Congo, akithibitisha ni silaha muhimu ya kikosi cha kocha Tarik Sektioui.

Lamlioui ameonekana kuwa mwepesi kufunga hata akiwa na mwanya mdogo, jambo ambalo litawalazimu mabeki wa Madagascar kuwa makini kila dakika.

Hata hivyo, mafanikio ya Morocco hayawezi kutenganishwa na ubunifu wa kiungo wao, Youssef Belammari. Mchezaji huyu mwenye miaka 27 ndiye kiungo wa kati anayeendesha mashambulizi. Amekuwa akisahaulika na wengi, lakini mchango wake ni mkubwa, ametoa asisti mbili hadi sasa na alikuwa mchezaji bora wa mechi ya nusu fainali dhidi ya Senegal.

Katika fainali hii, vita kubwa itakuwa kati ya Belammari na kiungo Nicolas Randriamanampisoa wa Madagascar. Nicolas, anayejulikana kama ‘Injini ya Barea’, ndiye roho ya timu ya Madagascar. Katika nusu fainali dhidi ya Sudan, alionesha kiwango cha juu kwa asilimia 88 ya pasi sahihi na kurejesha mipira iliyopotea mara 10, akijihakikishia tuzo ya mchezaji bora wa mechi.

Mbali na huyo, jina linalotikisa mitaa ya Antananarivo, huko Madagascar ni Toky Rakotondraibe. Mshambuliaji huyu chipukizi mwenye miaka 23 ndiye aliyefunga bao la dakika ya 116 lililoipeleka Madagascar kwenye fainali ya kwanza ya CHAN.

Hata kama hataanza katika kikosi cha kwanza, ubora wake wa kufunga mabao muhimu unamfanya kuwa kadi ya mwisho ya kocha Romuald Rakotondrabe kuweka historia Afrika.

Katika lango la Madagascar, ipo ngome ya uhakika chini ya uongozi wa kipa Ramandimbisoa ‘Toldo.’ Akiwa na umri wa miaka 29, Toldo amekuwa imara kwa timu yake, akifanya maajabu katika mechi ngumu ikiwemo dhidi ya Sudan na aliokoa mashuti manne ya hatari. Wachezaji wa Morocco inajua wazi kumpita Toldo si jambo rahisi.

Kama mechi hii itaenda hatua ya mikwaju ya penalti, Madagascar wataweka matumaini yao makubwa kwa Toldo, ambaye amekuwa jasiri na mtulivu hata kwenye dakika za mwisho. Uwepo wake unachochea imani ya wachezaji wenzake na mashabiki kwa jumla.

CHA 02

Kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano haya, mabingwa watapokea kitita cha dola milioni 3.5 (zaidi ya Sh9.1 bilioni), huku washindi wa pili wakipata Dola milioni 1.2 (Sh3.12 bilioni).

Timu itakayomaliza nafasi ya tatu itazawadiwa Dola 700,000 (Sh1.82 bilioni) na ile ya nafasi ya nne itajipatia Dola 600,000 (Sh1.56 bilioni).

CHA 03

Staa wa muziki wa Bongo Fleva, Zuchu pamoja na Eddy Kenzo na Savara wanatarajiwa kutumbuiza katika mechi hiyo ya fainali.

Zuchu anakuwa msanii wa pili atakayepafomu katika michuano hiyo baada ya awali Rayvanny kufanya shoo ya ufunguzi Kwa Mkapa Agosti 2.