SIMBA imewasili nchini alfajiri ya jana Ijumaa ikitokea jijini Cairo, Misri ilikoenda kuweka kambi ya mwezi ili kujiweka zaidi kwa msimu mpya wa mashindano, lakini kuna watu watatu wameshtua ndani ya ujio huo akiwemo kocha mkuu, Fadlu Davids.
Msafara huo wa Simba uliwasili ulirejea karibu wote isipokuwa kocha huyo na mastaa wengine wapya wa kikosi hicho walisajiliwa hivi karibuni na kuwasha moto huko Misri.
Wasaidizi wote wa Fadlu kuanzia Seleman Matola, Darian Wilken, kocha wa makipa Wayne Sandilands walishuka sambamba na wachezaji wao.
Katika msafara huo hakukosekana Fadlu peke yake, lakini viungo wapya wawili wa timu hiyo, Mohammed Bajaber na Neo Maema nao pia walikosekana na kulifanya Mwanaspoti kutafuta ukweli wa kukosekana huko kwa watu hao.
Taarifa kutoka Simba zinasema, Fadlu mara baada ya kumalizika kwa kambi yao alitimka sambamba na Maema wakirejea Afrika Kusini ambako wote wanatokea.
Simba licha ya Maema kuomba kutopumzika, lakini ilimpa muda wa kwenda kujikusanya kwao Afrika Kusini kabla ya kuja kuendelea na majukumu ya klabu hiyo iliyomsajili akitokea Mamelodi Sundowns.
“Kocha aliomba muda akaisalimie familia yake na tulimkubalia na atarejea hivi karibuni kabla ya kumalizika wiki hii,” alifafanua bosi mmoja wa Simba na kuongeza;
“Hata yule Maema unajua alitokea timu ya taifa na msichofahamu alipofika Misri makocha walimtaka kupumzika, lakini akakataa yeye mwenyewe, hata hivyo, tulipomaliza kambi akaomba arudi kuchukua kila kitu chake na kuaga familia.
“Nadhani kocha atakaporudi, watarudi na Maema unajua kila kitu kuhusu usajili wake kilimalizika akiwa timu ya taifa.
Aidha Bajaber licha ya Simba kutoeleza, lakini Mwanaspoti linafahamu kiungo huyo raia wa Kenya, amekwenda kupigwa picha maalum za utambulisho wa jezi mpya za Wekundu hao kwa msimu ujao.
Ikiwa Misri, Simba ilicheza jumla ya mechi nne za kirafiki ikishinda mbili, kupoteza moja na kutoka sare moja vilevile na sasa inajiandaa na mechi ya Ngao ya Jamii itakayopigwa Septemba 16 kabla ya kwenda Botswana kuvaana na Gaborone United ikiwa mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.