MWANARIADHA wa kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay, ameandika ukurasa mpya katika riadha nchini kwa kujenga kambi ya kisasa kwenye kijiji cha Madunga wilayani Babati, Mkoa wa Manyara.
Lengo la kambi hiyo ni kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana wa Kitanzania na kuandaa mashujaa wa kesho watakaoiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ikiwemo michezo ya Olimpiki.
Kambi ya Madunga imejengwa kwa viwango vya juu ikiwa na nyumba yenye vyumba, vitanda na vyoo vya kisasa, sehemu ya kuangalizia runinga kwa ajili ya kufuatilia mashindano ya kimataifa pamoja na intaneti ya bure kwa wanariadha kufuatilia programu za mafunzo.
Kwa sasa, kambi hiyo ina uwezo wa kuchukua wanariadha 30, lakini imeanza na vijana 15 wakiwemo wanne kutoka Kenya waliokuwa wakifanya mazoezi katika kambi maarufu ya Iten iliyopo Eldoret nchini Kenya.
Geay akifanya mahojiano maalumu na Mwanaspoti amesema ujenzi bado unaendelea na unatarajiwa kugharimu Sh400 milioni mpaka kukamilika, lakini cha kuvutia zaidi wanariadha waliopo sasa hawalipi chochote, wanakula, kulala na kupata usafiri wa kuwarudisha kutoka mazoezini bure.
Zaidi ya hapo, kampuni ya Asics imedhamini vifaa vya mazoezi ili kuhakikisha vijana hao wanaofanya mazoezi kwa ubora wa juu na kujiandaa kushindana na wakimbiaji bora duniani.
Nyota huyo anayeshikilia rekodi ya taifa ya marathoni na nusu marathoni, pia amejenga uwanja wa mazoezi Madunga mahali ambapo alizaliwa ambao unasaidia katika kuibua na kukuza vipaji vya riadha hasa katika wilaya za Babati na Mbulu.