Ilanfya kurejea kazini baada ya kupona

MSHAMBULIAJI wa JKT Tanzania, Charles Ilanfya anarejea kazini baada ya kukaa nje ya kazi kwa muda mrefu, kutokana na kuuguza majeraha ya goti la mguu wa kulia na kusababisha kucheza mechi moja msimu uliyopita.

Ilanfya aliumia Agosti 28, 2024 kwenye Uwanja wa Major Generali Isamuhyo, dakika chache baada ya kuingia kipindi cha pili mechi dhidi ya Azam, majeraha yaliyomuweka nje msimu mzima.

Baada ya kupona majeraha Ilanfya aliliambia Mwanaspoti kwamba ataungana na timu ikifika jijini Dar es Salaam ikitokea Arusha ilikoweka kambi kujiandaa na Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuanza Septemba 17 ambapo siku moja nyuma itachezwa mechi ya Ngao ya Jamii kati ya Simba na Yanga. “Kwa sasa naendelea vizuri, naiongojea timu ikitokea Arusha. Nafahamu nitakuwa na kazi ngumu ya kupambana katika mazoezi ili kurejesha ufiti na kupambania nafasi ya kucheza,” alisema Ilanfya na kuongeza:

“Timu ina mabadiliko kuna wachezaji wameondoka na wapya wameingia. Natarajia kuuona ushindani mkali ambao utasaidia kila mchezaji kuonyesha kiwango chake ili kumshawishi kocha kupata namba.”