Kibwana afafanua ishu ya kiungo Yanga

BAADA ya kuwapo kwa taarifa za kiungo mshambuliaji wa Yanga Princess, Aregash Kalsa kuachwa na timu hiyo, mratibu wa kikosi hicho Kibwana Matokeo amesema nyota huyo bado yupo Jangwani.

Kumekuwapo na taarifa mitandaoni zinazodai kwamba mchezaji huyo anayetumia mguu wa kushoto amejiunga na RS Berkane ya Ligi Kuu ya Wanawake Morocco.

Kalsa alijiunga na Yanga Princess msimu uliopita akitokea C.B.E ya Ethiopia aliyoisaidia kunyakua taji la Cecafa kwa wanawake.

Akizungumza na Mwanaspoti, Matokeo amesema kiungo huyo ana mkataba wa mwaka mmoja na leo anatarajiwa kuwasili nchini kutoka Ethiopia.

Ameongeza kuwa taarifa za kuachwa zinazozagaa mitandaoni wameziona na viongozi hawana presha kwani bado ana mkataba na Wananchi.

“Sisi tumeziona (hizo taarifa) na tumeshangaa imekuwaje. Leo (jana) anaingia nchini na atajiunga na wenzake kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya,” amesema Matokeo na kuongeza:

“Akifika atapiga picha na jezi mpya kwa sababu hatutatumia zilizopita zilikuwa na mdhamini Sportpesa tupo kwenye harakati za kutafuta mdhamini mpya.”

Kalsa msimu uliopita alicheza mechi tisa akifunga mabao matatu na asisti mbili akiingia dirisha dogo. Huyo ni mmoja wa wachezaji vipenzi vya mashabiki wa timu hiyo na mara kadhaa aliyekuwa kiungo wa Yanga, Aziz KI amekuwa akimtaja kuwa mmoja wa wachezaji bora upande wa wanawake.