Kina Kapombe kuikosa Gor Mahia Simba Day

NYOTA wa Simba waliokuwa katika kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kucheza michuano ya CHAN hawatakuwa sehemu ya mchezo wa tamasha la Simba Day kati ya Simba na Gor Mahia, Septemba 10.

Wacheza wa Simba ambao walikuwa kwenye kikosi cha Stars ni Shomari Kapombe, Yusuf Kagoma, Yakuob Suleiman, Abdurazack Hamza na Wilson Nangu.

Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids amesema wachezaji walikuwa na wiki nne nje ya Dar es Salaam na sasa wamerejea akitoa siku tatu za mapumziko na watarudi kambini baada ya muda huo kujiandaa na tamasha hilo.

“Tumekuwa nje ya ya Dar es Salaam kwa wiki nne tulikuwa na kambi yenye mazoezi ngumu, hivyo nimetoa siku tatu za mapumziko kwa wachezaji wakifikiria kile walichokipata na tutakutana kabla ya siku ya Simba ‘Simba Day’,” amesema na kuongeza:

“Kuna wachezaji wetu hatukuwa nao kabisa kutokana na majukumu ya kitaifa wakiitumikia Taifa Stars na watakuwa kwenye jukumu la kitaifa tunaweza tusiwe nao siku ya Simba Day, maana baada ya Simba Day tutakuwa na siku chache za kujiandaa na mechi ya kimataifa.”

Amesema uzoefu wake katika timu kubwa huwa wanakuwa na ratiba ngumu wakicheza mechi kila baada ya siku tatu na kusafiri umbali mrefu na ni muhimu katika maandalizi ya msimu sio kucheza kwa dakika zote 90, bali  kuangalia ratiba ya mechi kucheza mbili au tatu katika ligi.

“Kuna wakati nawapa presha makusudi wachezaji kwa kuwatia hasira, hasa wachezaji wapya nione wanaweza vipi na je wataweza kukabiliana na presha za mashabiki wanaopaza sauti kuomba kocha nimtoe mchezaji fulani… kuona je watahimili au watatetemeka? Hayo ndio mambo muhimu ninayoyafanya kuwaandaa wachezaji kabla ya msimu kuanza.”