KKKT Usharika wa Forest Mbeya kwafukuta, gari la kwaya kuu latajwa

Mbeya. Mgogoro umeibuka katika Kanisa la Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Tanzania (KKT) Dayosisi ya Konde Usharika wa Forest jijini Mbeya baada ya waumini kupinga uamuzi wa kusimamishwa kwa baadhi ya viongozi wao na Kwaya Kuu.

Imeelezwa kuwa Novemba mwaka jana, 2024, kanisa hilo lilipokea waraka kutoka jimboni kutaka kupunguzwa idadi ya Kwaya ndani ya usharika huo kubaki tatu.

Katika Kwaya zilizotajwa kupunguzwa, Kwaya Kuu haikuwamo, huku za kufutwa ikiwa ni Kwaya Safina na Hosiana lakini uongozi wa kanisa hilo umetaka Kwaya Kuu kufutwa na wanakwaya kujisajili upya.

Awali, katika kwaya tano zilizopo usharikani hapo ni Kwaya Kuu Forest, Kwaya Uinjilisti, Kwaya Hosiana, Kwaya Safina, Kwaya Vijana na Kwaya Uwaki.

Wakizungumza leo Agosti 30 Kanisani hapo, baadhi ya waumini wamesema hawakubaliani na uamuzi wa uongozi wa kanisa hilo wakidai kuwa Kwaya Kuu ina muda mrefu wa miaka 45 tangu kuanzishwa kwake.

Katibu wa Kwaya kuu, Julius Mwaikusi amesema barua iliyokuja kutoka Dayosisi ilielekeza kwaya zipunguzwe zibaki tatu, lakini imekuwa tofauti na utekelezaji hali iliyoleta taharuki na sintofahamu.

“Lakini imeenda mbali wakadai tusimamishwe kazi ikiwa ni Mwaikusi, Yonah Mwaisango, Michael Mwangonji na Petro Kyando na hakuna sababu ya kusimamishwa kwao,” amesema katibu huyo.

Naye Mwalimu wa Kwaya Kuu, Yonah Mwaisango amesema sababu kubwa inayoonesha kuamsha mgogoro ni baada ya kwaya hiyo kununua gari ilhali viongozi wa kanisa hawakutarajia.

Amesema pamoja na kusimamishwa kwao, lakini wamefuatilia kwa viongozi wa kanisa hilo bila mafanikio na kwamba hakubaliani na uamuzi huo kwani hakuna sababu zozote za msingi.

“Tunaomba kiongozi yeyote aingilie kati kumaliza mgogoro huu, kesho Jumapili tutaingia kanisani na kufunga muziki ili watufukuze tujue hatima yetu,” amesema Mwaisango.

Makamu Katibu wa Kwaya Kuu, Rehema Ibanje amesema wamesikitishwa sana na wito wa kanisa hilo juu ya uamuzi huo, jambo ambalo limewapa sintofahamu haswa kusimamishwa kwa viongozi na kujisajili upya.

“Zaidi wanatuambia mali za Kwaya Kuu zikabidhiwe kwa halmashauri hali ambayo ni tofauti kwa kuwa hakuna mchango wowote wa mtu zaidi ya sisi, tulichogundua ni kwamba wanataka kuwapa wengine na hatukubali,” amesema Rehema.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa njia ya simu, Mkuu wa Jimbo la kanisa hilo, Lusajano Sanga amesema hajapata taarifa za mgogoro huo akieleza kuwa anasubiri taarifa kutoka kwa mchungaji wa kanisa hilo.

“Sijajua kinachoendelea, sijaambiwa chochote na mchungaji ili aniambie kama kuna tatizo nijue tutafanyaje,”amesema Sanga.