Magu Yadhihirisha Kuelewa Ilani ya CCM 2025/2030 – Global Publishers



WANANCHI wa Magu wamemuonesha wazi Mgombea Mwenza wa Urais kupitia CCM, Balozi Dk Emmanuel Nchimbi kuwa wanaifahamu vyema Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2025/2030 baada ya kuielezea kwa ufasaha mbele yake.

Akizungumza na mamia ya wananchi wa wilaya hiyo waliojitokeza kumpokea, Nchimbi aliwataka waelezee hotuba ya mgombea urais Samia Suluhu Hassan kuhusu Ilani hiyo, hususani katika siku 100 za mwanzo za serikali ijayo iwapo CCM itapewa ridhaa ya kuongoza. Wananchi hao walitaja kwa ufasaha ahadi zilizotolewa na Samia ikiwemo ajira mpya kwa walimu wa masomo ya sayansi, bima ya afya kwa wote, marufuku ya kizuizi cha maiti kwa sababu ya gharama, pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mwanza hadi Isaka.

Katika hotuba yake, Nchimbi alieleza kuwa ndani ya miaka minne ya uongozi wa Rais Samia, maendeleo makubwa yamepatikana Magu ikiwemo ongezeko la vituo vya afya kutoka vitano hadi saba, zahanati kutoka 34 hadi 43, shule za sekondari kutoka 21 hadi 41, na madarasa kutoka 268 hadi 780. Pia huduma ya maji imeongezeka kutoka asilimia 53 hadi 63, umeme umefika vitongoji 136, na barabara za lami zimefikia kilomita 175, hatua ambazo alisema zimeifanya Magu kuwa mfano wa maendeleo ya vijijini na mijini.