Mahakama yaipa nafuu Chadema | Mwananchi

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Manyara, imekubali maombi ya Bodi ya Wadhamini wa Chadema ya kufungua shauri la maombi ya mapitio kupinga uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, aliyetengua uteuzi wa viongozi wa sekretarieti ya chama hicho.

Vilevile, imesimamisha uamuzi wa msajili huyo wa Mei 27, 2025 uliozuia Chadema kuendelea kupokea ruzuku, kusubiri uamuzi wa mapitio ya Mahakama katika maombi hayo.

Wajumbe wanane wa sekretarieti ya Kamati Kuu ya Chadema waliothibitishwa na Baraza Kuu la chama hicho, Januari 22, 2025 ni Katibu Mkuu, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu (Bara), Amani Golugwa na Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Ali Ibrahimu Juma.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Dk Rugemeleza Nshala; Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu na Hafidh Ally Saleh ambao ni wajumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.

Uamuzi huo umetolewa Agosti 28, 2025 na Jaji Devotha Kamuzora aliyekubali hoja mbili za waombaji walioomba ruhusa ya kufungua maombi ya marejeo na Mahakama itoe zuio la amri ya msajili.

Jaji Kamuzora amesema mahakama inatoa siku 14 kwa bodi hiyo kuwasilisha maombi kama ilivyoainishwa kisheria.

Maombi hayo ya madai yamewasilishwa mahakamani na bodi hiyo dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Katika hukumu hiyo iliyowekwa kwenye mtandao wa Mahakama Kuu wa TanzLii, waombaji waliomba ruhusa kufungua maombi ya marejeo kufuatia amri ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kuomba zuio la utekelezaji wa amri alizozitoa Mei 27, 2025.

Msajili alitoa amri ya kusitisha kutoa ruzuku kwa chama hicho hadi watakapotekeleza maelekezo ya ofisi yake huku akieleza Chadema haikuwa na viongozi wanaoweza kusimamia mapato, matumizi na marejesho ya fedha hizo za umma.

Msajili alielekeza kuitishwa Baraza Kuu jipya la Chadema lenye akidi stahiki ili kufanikisha uteuzi upya wa viongozi hao kwa mujibu wa katiba ya chama hicho, sheria ya vyama vya siasa na kanuni zinazohusika.

Chadema kupitia kikao cha Januari 22, 2025 kilithibitisha baadhi ya viongozi na wajumbe wake katika nafasi za sekretarieti na kamati kuu.

Baadaye aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho wilayani Mwanga, Lemburus Mchome alilalamikia kikao hicho akidai akidi haikutimia.

Ofisi ya msajili ilipata malalamiko kutoka kwa Mchome akipinga uhalali wa kikao hicho.

Mleta maombi aliwakilishwa mahakamani na mawakili Mpale Mpoki, Nyaronyo Kicheere na Thadei Lister, huku wajibu maombi wakiwakilishwa na mawakili sita wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Mark Mulwambo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola.

Wakili Mpoki aliwasilisha barua inayopingwa iliyotolewa Mei 27, 2025 akieleza maombi yao yamewasilishwa kwa wakati, akieleza bodi ya wadhamini moja ya majukumu yake ni kusimamia na kudhibiti mali zote zinazohamishika na zisizohamishika za Chadema zikiwemo fedha, hivyo ina masilahi katika shauri hilo.

Aliiomba mahakama kutoa ruhusa ya kufanyika marejeo ya uamuzi wa msajili na kutoa amri ya kusitisha utekelezaji wa barua yake inayozuia viongozi kujishughulisha na mali za Chadema wala kitu chochote.

Aliiomba mahakama viongozi waruhusiwe kuendelea na majukumu yao na fedha zitolewe akieleza shughuli za chama hicho zinadumazwa kwa barua hiyo.

Akijibu hoja hizo Wakili Kalokola alipinga maombi hayo kwa sababu mbili, akidai kulikuwa na suluhisho mbadala kwa mwombaji na pia hakuonyesha masilahi ya kutosha juu ya suala hilo.

Akizungumzia hoja ya masilahi ya umma, aliiomba mahakama isitoe nafuu inayoombwa kwani hakuna uongozi, ruzuku kwa chama cha siasa ambacho pia ni mfuko wa umma kuna uwezekano wa kusimamiwa vibaya na hakutakuwa na mtu wa kuwajibishwa.

Baada ya kupitia mawasilisho ya pande zote mbili, masuala ambayo mahakama iliangalia ni iwapo ombi limeonyesha masharti muhimu ya kutoa ruhusa ya kuomba mapitio ya mahakama, na iwapo mwombaji ana sababu za kutosha za kutoa amri ya kusitishwa uamuzi wa mjibu maombi wa kwanza (Msajili).

Jaji Kamuzora amesema kama ilivyowasilishwa na wakili wa mwombaji, kanuni elekezi imeweka wazi miongoni mwa masuala ya kuzingatiwa ni iwapo maombi yamewasilishwa ndani ya kipindi cha miezi sita, kama kuna kesi inayoweza kubishaniwa inavyostahili na kuamuliwa.

Kuhusu masilahi ya kutosha, Jaji Kamuzora amesema anakubaliana na hoja za wakili Mpoki kuwa kwa mujibu wa ibara ya 8 ya katiba ya Chadema mwombaji ana wajibu wa kusimamia mali zote za Chadema zinasohamishika na zisizohamishika.

Amesema na moja ya mali ya Chadema ni ruzuku inayotolewa kwa ajili ya shughuli za chama, hivyo mwombaji huyo ana masilahi na ameridhika kwamba ameonyesha kuwa na mamlaka sahihi ya kuwasilisha ombi hilo.

Jaji Kamuzora baada ya kupitia hoja zote alikubaliana na maombi hayo kwamba yana mashiko na yanakubaliwa.

Mahakama ilitoa muda wa siku 14 kuwasilisha maombi hayo pamoja na kusitisha amri ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya Mei 27, 2025 hadi maombi yaliyokusudiwa ya mapitio ya mahakama yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Golugwa, amesema wamepokea uamuzi wa mahakama na wanajipanga kumuandikia msajili barua kudai malimbikizo ya ruzuku aliyoizuia.

“Tumeyapokea maamuzi hayo ambayo kisingi ni haki tuliyostahili na tunataka Msajili wa Vyama vya Siasa aturejeshee malimbikizo ya ruzuku ambayo alizuia. Mnyika amenipa maelekezo nipeleke barua rasmi kwa msajili,” amesema na kuongeza:

“Tunaenda kudai malimbikizo ya ruzuku tangu alipositisha mpaka sasa ili shughuli za chama ziendelee.”