Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezielekeza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Wizara ya Nishati kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha magereza yote nchini yanaunganishwa na mfumo wa nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2027.
Majaliwa amesema hatua hiyo inalenga kuboresha mazingira ya wafungwa, kulinda afya za watumishi na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupunguza matumizi ya mkaa na kuni, ambayo ni chanzo kikuu cha uharibifu wa mazingira.
Majaliwa ametoa maelekezo hayo leo, Agosti 30, 2025, wakati wa uzinduzi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia magerezani, uliofanyika katika viwanja vya Gereza la Karanga, mkoani Kilimanjaro.
Amezitaka wizara hizo kuweka mikakati madhubuti ya utekelezaji wa agizo hilo ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya miundombinu inayohitajika, gharama na vyanzo vya nishati safi vinavyofaa kwa maeneo mbalimbali nchini.
“Wizara ya Mambo ya Ndani mshirikiane na Wizara ya Nishati, hakikisheni magereza yote nchini yanaunganishwa na mifumo ya nishati safi ifikapo mwaka 2027, mpaka gereza la kijijini liwe linapika kwa kutumia nishati safi,” amesema Majaliwa.
Kuhusu sekta binafsi, Majaliwa amesema: “Sekta binafsi, ikiwemo mama zetu, kwa yoyote anayefanya biashara hii ongezeni ubunifu na muwekeze teknolojia nafuu na salama kwa ajili ya kuweza kupata nishati hizi za kupikia ili tuwafikie wananchi wetu kule kijijini walipo, wananchi wengi watumie nishati safi ya kupikia, hili ni suluhisho bora kwa afya na mazingira.
“Nataka niwaambie tunaendeleza bidhaa hizi na kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao unaharibu mazingira yetu na afya za wananchi wetu.”
Pamoja na mambo mengine, ameyataka mashirika ya maendeleo na taasisi zilizopo za kiserikali kuendelea kushirikiana na Serikali ili kupanua mpango huo wa nishati safi hadi shule za bweni, hospitali na taasisi nyingine zilipo nchini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini, Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu amesema tayari wameshafunga mifumo ya nishati safi ya kupikia katika kambi 22 za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ndani ya mikoa 14 nchini.
“Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya nishati safi ya kupikia ambapo ni sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa Taifa kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Kingu.
Aidha, amesema kwa sasa wanaendelea na mradi wa kusambaza gesi asilia kwa ajili ya kupikia majumbani katika mikoa ya Pwani na Lindi.
Serikali imeandaa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao unatoa mwelekeo wa nchi wa kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ili kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.