*Awaomba wananchi wachague wagombea wa CCM Uchaguzi Mkuu Oktoba 29
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mvomero
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesema kwamba Tanzania ijayo itakuwa nchi yenye neema itakayotekeleza miradi ya maendeleo bila kutegemea fedha za mikopo mikubwa huku wananchi wakipata huduma bora za kijamii kama elimu,umeme, afya,maji na miundombinu mbalimbali.
Amesema kwamba kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeweka mikakati na mipango mbalimbali inayokwenda kuifanya Tanzania kuwa na maendeleo makubwa sambamba na kuondoa changamoto zinazowakabili Watanzania.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ambako anaendelea na kampeni za kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu utaokafanyika Oktoba mwaka huu Dk.Samia amesema anaiona Tanzania iliyojaa neema kuelekea dira 2050 na safari hiyo inaanza na miaka mitano ijayo ya uongozi wake.
Amesema ili kufikia maendeleo hayo amewaomba wananchi kukipigia kura CCM kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka huu ili kufanikisha neema hiyo.
Akieleezea zaidi Tanzania amewaomba wananchi kusimama pamoja kuiunga mkono CCM ili iendelee na kasi kujenga Tanzania tunayoitaka.
“Tukifika mwaka 2050 (kwa mujibu wa dira ya maendeleo ya taifa 2050) tuwe tumeifika Tanzania yenye uchumi wa kipato cha kati ngazi ya juu. Hakuna Mtanzania atakayelia kukosa huduma za afya, elimu wala kukosa umeme.
“Tutakuwa na Tanzania ambayo uchumi wake utasimama kujitegemea, hatutaishi wala kufanya shughuli za maendeleo kwa mikopo mikubwa. Na hiyo safari tunaanza miaka mitano inayokuja,”amesema Dk.Samia na kusisitiza “malengo ya Serikali ni kuwa na Tanzania ambayo haitakuwa na changamoto ya huduma muhimu za kijamii.”
Hata hivyo mgombea Urais Dk. Samia ameeleza wazi kwamba ili kufikia azma hiyo, ifikapo Oktoba 29 mwaka huu, wananchi wajitokeze kwa wingi katika vituo vya kupiga kura kukichagua Chama Cha Mapinduzi.
Akiwa katika mkutano huo wa Wilaya ya Mvomero Dk.Samia amewapongeza wananchi wa wilaya hiyo kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani 394,354 hadi kufikia zaidi ya tani 400,000.
Kwa upande wa mazao ya kibiashara yakiongezeka kutoka tani 400,000 hadi tani zaidi ya 500,000 huku akifafanua kuwa ongezeko hilo limetokana na upatikanaji pembejeo, mbegu bora na zana za kilimo.
Akizungumza kuhusu migogoro baina ya wakulima na wafugaji, Dk. Samia ameeleza kupitia kampeni ya Tutunzane imewezesha kuleta utulivu, kupendana na amani.
“Pia tumeendelea kushirikiana na wafugaji wetu na tumeongeza minada ya mifugo kutoka mitatu hadi mitano, tumejenga machinjio Matano, mashamba darasa yameongezeka kutoka shamba moja hadi 42.
“Hii ni hatua kubwa nzuri, wananchi ni mashahidi wa kazi zilizofanywa na serikali ya CCM,” amesema Dk.Samia katika mkutano huo uliofanyika mapema leo Agosti 30,2025.
Ametumia pia nafasi hiyo kuahidi kuwa Serikali atakayoiunda baada ya kumalizika kwa Uchaguzi mkuu itakamilisha ujenzi kituo cha afya Dawaka, zahanati, kutekeleza bima ya afya kwa wote, kujenga na kuboresha shule za sekondari ikiwemo kukamilisha vyumba 31 vya madarasa ya shule za msingi.