Miradi ya Sh164 bilioni kutembelewa na mbio za mwenge

Geita. Miradi 61 yenye thamani ya zaidi ya Sh164 bilioni inatarajiwa kutembelewa, kukaguliwa, kuwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka huu mkoani Geita, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya asilimia 500 ya thamani ya miradi iliyotembelewa mwaka 2024.

Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigela ameyasema hayo leo Septemba 30, 2025, wakati akitoa taarifa za ujio wa Mwenge huo utakaoanza kukimbizwa mkoani humo Septemba mosi, 2025.

Amesema mwaka jana, Mwenge wa Uhuru ulipita mkoani Geita na kukagua miradi 65 yenye thamani ya Sh32 bilioni, ikihusisha sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.

Baadhi ya miradi hiyo ilikuwa ni ujenzi wa shule mpya, vituo vya afya, visima vya maji pamoja na miradi ya vijana na wanawake.

Kwa mujibu wa Shigela, mwaka huu kiwango cha uwekezaji kimeongezeka kwa zaidi ya asilimia 500 ikilinganishwa na mwaka uliopita.

“Mwenge wa mwaka huu si tu utakagua na kuzindua miradi, bali pia utahamasisha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025,” amesema Shigela.

Ameongeza kuwa mbio za Mwenge wa mwaka huu zinaongozwa na kauli mbiu: “Jitokezeni kushiriki uchaguzi mkuu 2025 kwa amani na utulivu,” ikilenga kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura, kusikiliza sera za vyama vya siasa na kuchagua viongozi kwa amani na utulivu.

“Kampeni tayari zinaendelea, na tumejipanga kuhakikisha kila mgombea anafanya kampeni kwa uhuru bila bughudha. Ni wajibu wetu kuimarisha mshikamano na kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi,” amesema Shigella

Mkazi wa Shilabela mjini Geita, Musa Ndoshi, amesema ujio wa Mwenge wa Uhuru ni kichocheo cha maendeleo kutokana na mkoa kujipanga kila mwaka kuwa na miradi ya kuzinduliwa.

Kwa upande wake, Agness Mabula mkazi wa Nyankumbu, amesema Mwenge wa Uhuru umekuwa ukitumia gharama kubwa kuliko baadhi ya miradi inayotekelezwa, na ameshauri serikali kuufanya uwe wa kukimbizwa kila baada ya miaka mitano ili kuenzi historia badala ya kila mwaka.