MOROCCO imeweka rekodi mpya katika michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya kutwaa taji la tatu ikiwa ndiyo timu iliyochukua mara nyingi zaidi.
Rekodi hiyo imeiweka kufuatia ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Madagascar katika mchezo wa fainali uliochezwa leo Agosti 30, 2025 kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Moi uliopo Kasarani, jijini Nairobi nchini Kenya.
Morocco iliyotwaa ubingwa wa CHAN mwaka 2018 ilivyokuwa mwenyeji kisha 2020 na sasa ambayo imefanyika kwa ushirikiano wa nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda, haikuwa rahisi kufikia mafanikio hayo kwani ililazimika kutokea nyuma baada ya Clavin Félicité Manohantsoa kuifungia Madagascar bao la kwanza dakika ya tisa akimalizia pasi ya Mika Nantenaina Razafimahatana.
Morocco ilijiuliza maswali mengi na hatimaye dakika ya 27, Youssef Mehri akaitumia vizuri pasi ya Khalid Baba kusawazisha bao hilo.
Dakika moja kabla ya kwenda mapumziko, Oussama Lamlioui aliiweka mbele Morocco akiifungia bao la pili na kufanya dakika 45 za kwanza kumalizika ubao ukisoma Madagascar 1-2 Morocco.
Toky Niaina Rakotondraibe ambaye alifunga bao pekee wakati Madagascar ikiichapa Sudan 1-0 na kufuzu fainali ya michuano hiyo kwa mara ya kwanza, alirudisha matumaini kufuatia kuisawazishia timu hiyo dakika ya 68 kutokana na pasi ya mfungaji wa bao la kwanza, Clavin Félicité Manohantsoa.
Matumaini hayo yalidumu kwa takribani dakika 12 kwani Madagascar wakati ikipambana kusaka bao la kuongoza, mfungaji bora wa CHAN 2024, Oussama Lamlioui akamchungulia kipa Ramandimbisoa aliyesogea kidogo mbele, akaachia shuti kali la umbali wa yadi 40 na mpira kutinga wavuni.
Bao hilo la ushindi lililofungwa dakika ya 80 likiwa ni bao lake la sita kwenye mashindano hayo, lilitokana na pasi ya nahodha Mohamed Rabie Hrimat na kufanya matokeo hadi mwisho kuwa Madagascar 2-3 Morocco.
Kwa kutwaa ubingwa huo, Morocco imekabidhiwa kombe, medali ya dhahabu na zawadi ya dola milioni 3.5, huku Madagascar ikiambulia medali ya fedha na kiasi cha dola milioni 1.2.
Kwa upande wa zawadi binafsi, mbali na Oussama Lamlioui kuwa kinara wa mabao akifunga sita, nahodha wa Morocco, Mohamed Hrimat ametwaa Tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashindano huku Senegal iliyokuwa bingwa mtetezi iliyomaliza nafasi ya tatu, imebeba Tuzo ya Mchezo wa Kiungwana (Fair Play Award) na Marc Diouf wa Senegal akiwa Kipa Bora.