Plastiki zilivyobadili maisha ya Mahanji aliyekatwa mguu kwa kisukari

Shinyanga. Katika juhudi za kulinda mazingira, Mahanji Seif, mkazi wa Kata ya Ndala, mkoani Shinyanga, ameibuka na ubunifu wa kutengeneza bidhaa kwa kutumia chupa za plastiki.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake, Mahanji ameeleza alilazimika kuanzisha mradi huo baada ya kukatwa mguu kutokana na ugonjwa wa kisukari, hali iliyomfanya ashindwe kuendelea na shughuli zake za awali.

“Nilipopata matatizo ya kisukari mguu wangu uliharibika na kupelekea kukatwa. Hapo maisha yangu yakabadilika kabisa, sikuweza kufika sehemu nilizokuwa nafanya biashara. Ndipo nilipoamua kuanzisha mradi ambao naweza kuufanya nikiwa nyumbani,” amesema.

Anaeleza wazo la kutengeneza bidhaa kwa kutumia plastiki lilitokana na kumbukumbu ya kutumia ukindu kusuka mikeka.

“Niliposhindwa kuendelea na biashara sokoni, maisha yalikuwa magumu. Hata mtoto wangu alilazimika kuacha chuo kwa kukosa ada. Nikawaza, badala ya ukindu, naweza kutumia chupa za plastiki kusuka mikeka. Hapo ndipo safari hii ilipoanza,” anasema.

Anasema kwa kufanya shughuli hizo sasa anaweza kumudu gharama za kuendesha maisha ya familia yake yenye watu 11.

Mahanji anaeleza kwa kutumia chupa za plastiki hutengeneza bidhaa kama vile mikeka, vikapu, uzio na vyombo vya kuhifadhia taka. Bidhaa hizo huuza kati ya Sh20, 000 na Sh40,000 kulingana na ukubwa wake.

Lemida Hussein, mkewe Mahanji anaeleza mradi huo umebadilisha hali ya familia baada ya kipindi kigumu.

“Baada ya baba kukatwa mguu maisha yalikuwa magumu. Nilitegemea kibanda changu cha matunda sokoni ambacho kilikuwa hakitoshi. Mradi huu umesaidia kuongeza kipato na kuboresha maisha yetu,” anasema.

Wateja wake pia wameonyesha kuridhishwa na bidhaa hizo, Rukia Iddy, mmoja wa wateja hao akisema: “Nimenunua mkeka kwa sababu hauozi na unanisaidia kuzuia vumbi sokoni. Pia nautumia kuanikia dagaa, umekuwa msaada mkubwa kwangu.”

Mahanji anasema hukusanya chupa za plastiki kwa msaada wa watoto wake au kwa kuzinunua kutoka kwa wakusanyaji kwa Sh200 kila chupa 10.

Baada ya kuzipanga kwa rangi, hukata vipande kwa mkasi au kisu, huvinyoosha vipande hivyo na kuanza kusuka mikeka.

Mkeka mmoja au kikapu anasema huweza kumchukua hadi siku 15 kukamilisha kazi ya utengenezaji.

Vilevile, hutengeneza uzio kwa kuunganisha chupa hizo kwa sindano na uzi wa timba. Uzio huo hutumika kuzungushia bustani, kulinda miti midogo na kufugia kuku au bata.

Mbunifu huyo anasema yupo tayari kufundisha mbinu hizo bure kwa mtu atakayekusanya chupa na kufika nyumbani kwake.


Plastiki zilivyobadili maisha ya Mahanji aliyekatwa mguu kwa kisukari

“Ajira zipo, watu wasilalamike. Hata vijana wana nguvu wanaweza kujipatia kipato kwa njia hii n ahata kulinza mazingira. Ni kazi ambayo hata wazee wanaweza kufanya wakiwa nyumbani,” anasema.

Hata hivyo, ameiomba Serikali na taasisi binafsi kumsaidia kupata vitendea kazi kama vile bajaji kwa ajili ya kukusanya chupa na mashine za kisasa za kukata plastiki ili kurahisisha kazi na kuongeza uzalishaji.

Ripoti ya Turning off the Tap (2023) ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) inaonya kuwa plastiki zimekuwa tishio kwa mazingira na afya za jamii duniani.

Ripoti hiyo inabainisha kuwa: “Bila hatua madhubuti, uzalishaji wa plastiki unaweza kuongezeka mara mbili ifikapo mwaka 2040, na kuongeza maradufu taka zinazoharibu udongo, vyanzo vya maji na maisha ya viumbe hai baharini.”

Ripoti inasisitiza kuwa plastiki zinazotupwa holela huchangia uchafuzi wa mazingira, kuathiri uzalishaji wa chakula na hata kuingia kwenye mnyororo wa chakula cha binadamu, ikipendekeza suluhisho ni kuwekeza kwenye shughuli mbadala za matumizi ya plastiki au bidhaa nyingine rafiki wa mazingira na mifumo ya kuchakata taka hizo, hasa katika kipindi hiki ambacho zinaongezeka nchini.

Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya mwaka 2023/24 inaonyesha thamani ya plastiki zilizoingizwa nchini imeongezeka kwa asilimia 5.2, kutoka Sh1.678 trilioni mwaka 2022/23 hadi Sh1.765 trilioni mwaka 2023/24.

Hii inaashiria ongezeko la plastiki zinazoingia nchini, ambazo zinahitaji mkakati wa kuzirejeleza katika matumizi mengine. Moja ya hatua za kuchukua ni kama ya Mahanji ya kuzitumia tena taka za plastiki.