Polisi, Chadema lugha gongana kuhusu madai ya Temba

Arusha. Jeshi la Polisi mkoani Arusha limekana tuhuma za Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha ) Kanda ya Kaskazini, Gasper Temba (30), anayedaiwa kutekwa jijini Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Arusha, Justine Masejo leo Jumamosi Agosti 30, 2025, imesema kuwa inamshikilia Temba kwa tuhuma za kughushi zinazomkabili jijini Dar es Salaam.

Taarifa ya Kamanda Masejo imekuja baada  zilizosambaa habari katika mitandao mbalimbali ya kijamii leo zikidai Temba ametekwa na watu wasiojulikana leo saa 10 jioni.

“Kuna taarifa inasambaa katika baadhi ya mitandao ya kijamii ikieleza Temba ametekwa jijini Arusha.Taarifa sahihi ni kwamba Temba mkazi wa Arusha hajatekwa, bali amekamatwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma zinazomkabili za kughushi nyaraka.”

“Tukio ambalo lilifunguliwa huko jijini Dar es Salaam na kwamba amekamatwa kwa mujibu wa sheria na taratibu nyingine za kisheria zinafuata,”imesema taarifa ya kamanda huyo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linatoa onyo kwa watu wanaotumia mitandao ya kijamii kuacha kusambaza taarifa ambazo hawana uhakika zinazoweza kusababisha taharuki katika jamii,” ameongeza.

Awali, jitihada za Mwananchi kuwapata viongozi wa Chadema Mkoa na Kanda ya Kaskazini ziligonga mwamba kutokana na simu zao kuita bila kupokewa.

Taarifa za awali zilidai Temba ametekwa na watu wasiojulikana ambao walimfunga pingu na kuondoka naye katika eneo moja jijini Arusha mbele ya benki yenye lindo la polisi.