RAIS SAMIA KUA MGENI RASMI KATIKA KILELE CHA WIKI YA USAFIRI ENDELEVU

:::::::

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha wiki ya maadhimisho ya usafiri endelevu ardhini, yatakayofanyika Novemba 26, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yanaratibiwa na Wizara ya Uchukuzi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), yakiwa na lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi na ujenzi wa miundombinu rafiki kwa mazingira katika sekta ya usafirishaji.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam baada ya kikao cha wadau wa usafirishaji, Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo, alisema maadhimisho hayo ya siku sita yataanza Novemba 24 hadi 29, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), yakibeba kaulimbiu isemayo: “Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji.”

Suluo alibainisha kuwa, siku ya kilele na ambayo pia ni siku rasmi ya maadhimisho hayo kimataifa ni Novemba 26, na mgeni rasmi atakuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

“Maadhimisho haya yanalenga kuunga mkono juhudi za Rais Samia katika kukuza matumizi ya nishati safi na usafiri rafiki kwa mazingira, huku tukisisitiza umuhimu wa ubunifu katika kuboresha sekta ya usafiri nchini,” alisema.

Aidha, Suluo aliwataka waandishi wa habari kutumia kalamu zao kwa uzalendo, kuhakikisha kuwa wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia maslahi ya taifa hasa katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29.

“Ni muhimu wanahabari kuepuka taarifa zenye mwelekeo wa kuchochea taharuki au kuvuruga amani ya nchi. Waendelee kuwa sehemu ya kudumisha utulivu kwa kulinda maadili ya taaluma yao,” aliongeza.

Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia imeweka mkazo mkubwa katika usimamizi wa sekta ya usafiri kwa kuzingatia misingi ya utawala bora na maendeleo endelevu, hali iliyowezesha kufanikisha hatua ya kuandaa maadhimisho hayo kitaifa.

Kwa mujibu wa LATRA, maonesho mbalimbali ya ubunifu, teknolojia za kisasa katika usafiri, na mijadala ya kitaalamu kuhusu usafiri endelevu yanatarajiwa kuwasilishwa katika kipindi chote cha maadhimisho hayo.