Siri nzito dili la Nangu, Yakoub

SIMBA imetua nchini alfajiri ya jana ikitokea Misri ilipoweka kambi ya maandalizi ya msimu mpya wa 2025-2026, lakini huku nyuma mabosi wa klabu hiyo wamefanya jambo moja lililowahakikishia kuwamiliki wachezaji wawili nyota kutoka JKT Tanzania.

Kama unakumbuka Mwanaspoti liliwafahamisha mapema Simba ilishamalizana na beki Wilson Nangu na kipa Yakoub Suleiman waliokuwa wakiitumikia Taifa Stars katika mechi ya fainali za CHAN 2024 na walikuwa wanasubiri wamalize jukumu la kitaifa wajiunge na timu hiyo.

Juzi usiku JKT iliwapa ‘thank you’ nyota hao kuashiria kila kitu kipo sawa na kwa taarifa yako tu, mabosi wa Simba wamemalizika kulipa zaidi ya Sh500 milioni ili kuwanasa na muda wowote kuanzia leo wanatarajiwa kutambulishwa rasmi na Wekundu wa Msimbazi hao.

Ipo hivi. Simba imelazimika kulipa Sh400 milioni kwa maafande, ikiwa ni Sh200 milioni kwa kila mchezaji, lakini imelipa pia fedha nyingine zinakadiriwa kuwa Sh50 milioni kwa JKU inayommiliki kipa Yakoub na nyingine zaidi ya hizo kwa wachezaji, japo viwango havijawekwa wazi.

Licha ya kutoa fedha hizo zaidi ya Sh500 milioni, Simba pia imewatoa kwa mkopo wachezaji watatu wa kikosi hicho kwenda JKT akiwamo beki David Kameta ‘Duchu’, kiungo Awesu Awesu na mshambuliaji, Valentino Mashaka.

Pia inadaiwa hata beki mpya aliyesajiliwa kutoka TMA Stars iliyopo Ligi ya Championship, Vedastus Masinde naye huenda akapelekwa kwa mkopo kwa maafande hao wa JKT, hii ni baada ya kupata uhakika wa kumtumia Nangu ambaye aliyerithiwa na beki huyo mara alipoondoka TMA.

Wachezaji hao watatu wametolewa na Simba kama sehemu ya masharti ya kuachiwa Nangu na Yakoub walioisaidia JKT Tanzania kumaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu katika nafasi ya sita, lakini wakiwa sehemu ya kikosi cha Stars kilichofika robo fainali ya Kombe la CHAN 2024.

Nyota hao wawili walioagwa JKT walikuwa wamesainishwa mikataba mipya hivi karibuni, ule wa Nangu ulikuwa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028, wakati wa Yakoub ni hadi 2027, hivyo Simba imelazimika kulipa kiasi hicho cha fedha kila mmoja kwa Sh200 milioni, mbali na fedha kwa JKU ambayo ni mwajiri wa Yakoub.

Utaratibu wa JKU anapouzwa mchezaji ambaye ni askari kama Yakoub inagawana pesa za dau la usajili pasu kwa pasu, kwa sababu licha ya kuruhusiwa kucheza ajira yake ipo pale pale.

Mwanaspoti limezinasa taarifa za ndani kutoka klabu hizo mbili za Simba na JKT zinazosema dili la wachezaji hao limekamalika na Yakoub amesaini mkataba wa miaka mitatu na tayari kaingiziwa kibunda chake akienda kuziba nafasi iliyuoachwa wazi na Ally Salim.

“Nangu pia amesaini mkataba wa miaka mitatu, hivyo Simba imetoa zaidi ya Sh500 milioni kukamilisha usajili wa wachezaji hao kwa kuzilipa JKT Tanzania, JKU na wachezaji wenyewe,” kilisema chanzo hicho na kuongeza; 

“Nangu na Yakoub wanatarajia kujiunga na timu ya Simba wakati wowote kuanzia sasa baada ya kurejea ikitokea Misri ambako ilipiga kambi kujiandaa na msimu mpya.”

Awali, Yanga ndio iliyokuwa ya kwanza kuhitaji huduma ya Yakoub kwa dau la Sh100 milioni ili kumsajili kwa mkataba wa miaka mitatu, ilishindikana haikuwa na masilahi kwa mchezaji.

Katibu wa JKU Khatib Shadhil, alipotafutwa na Mwanaspoti alisema: “Tunamtakia kila heri Yakoub katika majukumu yake mapya, tunaamini atakwenda kupambana na huduma yake kufanyika msaada kwa timu.”