Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, imebaini mapungufu katika miradi 11 ya maendeleo yenye thamani ya Sh6.68 bilioni mkoani Kilimanjaro.
Akitoa taarifa ya utekelezaji katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Musa Chaulo, amesema katika kipindi hicho taasisi hiyo ilifuatilia utekelezaji wa miradi 19 ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Sh8 bilioni, ili kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana.
Chaulo amesema miradi hiyo ni ya sekta za afya, elimu, ujenzi, maji na barabara na kati ya hiyo, miradi 11 yenye thamani ya Sh6.6 bilioni ilibainika kuwa na mapungufu na tayari ushauri umetolewa kwa wahusika ili kufanya marekebisho.
Aidha, amesema katika ufuatiliaji wa mradi pia walikagua ujenzi wa shule mpya ya sekondari Hedaru wilayani Same, yenye thamani ya Sh586 milioni na kubaini Sh136.5 milioni zilitumika bila kukatwa kodi ya zuio.
Ameongeza kuwa “baada ya kuingilia kati, halmashauri ilikatwa kodi hiyo na kufanikisha kuwasilishwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Sh9.9 milioni Mei 2025”.
Amesema kupitia ufuatiliaji huo pia taasisi hiyo imesaidia kuwasilishwa michango ya NSSF ya Sh1.7 milioni ya watumishi watatu wa kituo cha Tumaini Urban Health Centre Ltd, ambacho kilikuwa hakijaiwasilisa kwa zaidi ya miaka miwili.
Kwa upande wa malalamiko, Chaulo amesema katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2025, jumla ya malalamiko 97 yalipokewa, ambapo 50 yalihusu rushwa na 47 yalihusu masuala mengineyo.
“Kwa upande wa mashtaka, kesi 22 zimefikishwa mahakamani, kesi mpya nne zimefunguliwa, kesi ilizoshinda tatu na katika zinazoendelea kwenye mahakama mbalimbali mkoani Kilimanjaro ni mbili zinazohusu rushwa kubwa,” amesema Chaulo.
Amesema kupitia programu ya Takukuru Rafiki, iliibuliwa kero ya mwenyekiti wa Chama cha Ushirika Mwenge Shirimatunda kutoweka fedha za wanachama Sh986,000 katika akaunti ya chama tangu mwaka 2016.
“Baada ya ufuatiliaji, mwenyekiti huyo alirejesha fedha hizo Aprili 2025 na kuziweka kwenye akaunti ya chama hicho. Lakini pia katika kipindi hicho tumeweza kuzifikia kata 10 na jumla ya kero 115 zilibainika, ambapo kero 99 zilitafutiwa majawabu na 16 zinaendelea kushughulikiwa”.
Aidha, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Takukuru kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa hususani kuelekea uchaguzi mkuu mwaka huu akisisitiza matumizi ya Takukuru App katika kurekodi na kutuma taarifa.
“Tunaendelea kuelimisha jamii na makundi mbalimbali ili washiriki katika uchaguzi mkuu pasipo kujihusisha na vitendo vya rushwa”.
Baadhi ya wananchi mjini Moshi wamesema elimu dhidi ya rushwa ni muhimu hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, wakisisitiza kuwa vitendo vya rushwa vimekuwa kikwazo cha kuchagua viongozi wenye uwezo wa kweli.
Faith Mongi mkazi wa Moshi amesema matumizi ya Takukuru App ni nyenzo muhimu ya kuondoa hofu kwa wananchi wanaotaka kutoa taarifa za rushwa.