Tanesco yakamata watano kwa hujuma ya miundombinu Kahama

Shinyanga. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kanda ya Magharibi kwa kushirikiana na maafisa kutoka makao makuu, limewakamata wateja watano wanaodaiwa kuhujumu miundombinu ya shirika hilo kwa njia zisizo halali ikiwemo kuhamisha na kuchezea mita wilayani Kahama mkoani Shinyanga.

Tukio hilo limebainika kupitia operesheni maalum ya ‘Baini wajibika Okoa Mapato (BAOMA), iliyoendeshwa na shirika hilo kwa kushirikiana na vyombo vya usalama, ambapo jumla ya wateja 473 walikaguliwa.

Akizungumza leo Agosti 30, 2025 Mkuu wa TANESCO Kanda ya Magharibi, Felix Mwinuka, amesema, watuhumiwa walikutwa wakitumia umeme bila kupitia mita, wengine wakihamisha mita kutoka maeneo mengine na baadhi kuchezea mita zao ili kuepuka kulipa gharama halali za matumizi.

Amesema miongoni mwa makosa waliyoyabaini ni Pamoja na kuhamisha mita kinyume na utaratibu, kutumia umeme usiopita kwenye mita (Bypass), kuchezea mita hali iliyosababisha umeme kutosoma ipasavyo.

“Wateja hao tumewakabidhi kwa vyombo vya dola kwa hatua za kisheria,” amesema Mwinuka na kuongeza kuwa kitendo hicho ni hujuma dhidi ya miundombinu ya umma na kinyume na sheria.

Msimamizi wa usalama Tanesco kanda ya Magharibi Said Sombwe amesema operesheni hiyo inalenga kuhakikisha matumizi halali ya umeme na kuonya kuwa TANESCO itaendelea kuwafuatilia wahusika wote wa hujuma nchini.

Amesema “Tumejumuika kama timu kubwa kutoka makao makuu na kanda mbalimbali. Rai yangu kwa wananchi ni kufuata taratibu za TANESCO kwa kuwa mkono wa shirika ni mrefu, tutawafikia popote walipo.”

Miongoni mwa waliokamatwa ni Omega Nyuki mkazi wa Mhungula-Kahama, ambaye amekiri kununua mita haramu kwa Sh650,000 baada ya kusitishiwa huduma.

Nyuki pia alikuwa akiuza umeme kwa majirani zake kwa Sh100,000, hatua iliyosababisha kusitishiwa huduma kwa wote aliowaunganishia.

Amesema “Nilihitaji umeme baada ya kusitishiwa huduma. Kuna mafundi waliniletea mita iliyohamishwa, nilijua wanatoka TANESCO maana huwa nawaona wanaunganishia umeme watu wengine, nikainunua wakanifungia. Sikuwa na nia ya kuibia shirika. Nimekamatwa na niko tayari kwa lolote litakalotokea.”

Tanesco imesisitiza kuwa operesheni BAOMA itaendelea kote nchini na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa dhidi ya watu wanaohujumu miundombinu ya shirika hilo.