Usafiri Mbagala ni mwendo wa kiyoyozi, ‘ruti’ ya Morocco yaongezwa

Dar es Salaam. Wakati mabasi yaendayo haraka ‘mwendokasi’ kwa ajili ya Mbagala yakitolewa bandarini Dar es Salaam, tofauti na taarifa ya awali, sasa njia za safari zimeongezwa huku mabasi hayo yatakuwa na kiyoyozi na abiria wataweza kuperuzi mtandao wa inteneti bure.

Mbali ya hilo, idadi ya mabasi pia imeongezeka na kufikia 151.

Mabasi hayo yaliyokuwa yafanye safari kati ya Mbagala-Gerezani na Mbagala -Kivukoni, sasa yatakwenda pia Morocco, wilayani Kinondoni.

Vilevile, mabasi 52 yameongezwa na kufanya idadi ya yaliyowasili nchini hadi sasa kufikia 151. Usafirishaji abiria imeelezwa unatarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa, huku awali ilielezwa ungeanza Septemba Mosi, 2025.

Hayo yameelezwa jana Ijumaa Agosti 29, 2025 na  Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Dk Athuman Kihamia wakati wa kuyatoa mabasi hayo katika Bandari ya Dar es Salaam na kuyapeleka kwenye karakana iliyopo Mbagala Rangi Tatu.

Kazi ya kuyatoa mabasi hayo bandarini ilianza jana Agosti 29, saa tatu usiku.

Mradi huo wa awamu ya pili kutekelezwa ukitanguliwa na ule wa Kimara ulioanza mwaka 2016, kampuni ya wazawa ya Mofat ndiyo imepewa mkataba wa miaka miwili wa kuuendesha ikitarajia kuingiza nchini mabasi 255. Idadi ya yaliyokwisha kufika ni 152.

Hata hivyo, wakati mradi wa kwanza ulihitajika kuwa na mabasi 302, huu wa awamu ya pili unahitajika kuwa na jumla ya mabasi 755.

Inaelezwa ndiyo awamu yenye mabasi mengi kulinganisha na nyingine sita zitakazokuwapo katika miradi ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).

Kwa mujibu wa Dk Kihamia, katika uletaji wa mabasi hayo awamu ya kwanza 99 yalifika nchini Agosti 5, huku 52 yakiingizwa Agosti 26. Mengine 153 yanatarajiwa kuletwa katikati ya Oktoba na kufanya idadi kufika 255.

Dk Kihamia amesema tofauti na awali, mabasi hayo sasa yatatoa huduma Mbagala kwenda Gerezani, Mbagala kwenda Kivukoni na Mbagala kwenda Morocco.

“Mabasi haya 151 yatatoa huduma katika barabara hizo na tutayaelekeza kulingana na mahitaji ya usafiri kwa wakati husika, huenda eneo fulani likawa na uhitaji zaidi tukaachia magari 50 kwa wakati mmoja, hususani asabuhi watu wakienda kazini na jioni wakirejea majumbani. Kwa kuwa tuna mfumo wa kisasa wa kuongozea magari utakuwa ukituonyesha hayo yote,” amesema.

Amesema magari yote yakishawasili yatakwenda kutatua changamoto ya usafiri.

Dk Kihamia akizungumzia madereva, amesema wamepata mafunzo ya uhakika ya uendeshaji na ana imani hakutakuwa na ajali zinazosababishwa na uzembe kutoka kwao.

“Hata hivyo, ili hili lifanikiwe ni vema wananchi kuacha kutumia barabara za magari hayo kwa kuwa yanaenda haraka na yatakuwa mengi barabarani, hivyo ajali zinaweza kuwa nyingi zaidi kama hawatakuwa makini. Ni vema tukayalinda na kuyatunza mabasi haya, lakini na sisi tukajilinda na ajali za kujitakia wenyewe,”

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mofat, Muhammad Abdallah Kassim, ameshukuru namna Serikali ilivyoshirikiana nao kwa karibu kuhakikisha mabasi hayo yanatoka bandarini.

“Kwa kweli tunaishukuru Serikali ilivyokuwa bega kwa bega na sisi kuhakikisha tunayatoa mabasi haya ndani ya muda mfupi, kwani ingekuwa siyo ushirikiano wao huenda ingechukua muda zaidi ukizingatia yapo mengi,” amesema.

Amesema wamejipanga vilivyo katika utoaji huduma, akieleza ana imani abiria watazifurahia.


Usafiri Mbagala ni mwendo wa kiyoyozi, ‘ruti’ ya Morocco yaongezwa

Kassim amesema abiria watakaopanda mabasi hayo ukiacha kuwa yana viyoyozi, watapata huduma ya mtandao bure.

“Tumeshaongea na kampuni ya mtandao (anaitaja) kuhusu kufunga mtandao wa bure kwenye mabasi yetu, hivyo mtu ukipanda humu hata kama hauna bando utaweza kuperuzi kama kawaida,” amesema.

Kassim amesema kwa watakaoishiwa chaji wataweza kuchaji ndani ya mabasi hayo.

Vilevile, katika kudhibiti matukio ya wizi ndani ya mabasi kumefungwa kamera, lengo likiwa kuhakikisha usalama.

“Gari zetu ni za kisasa na zimezingatia matakwa ya usafiri wa kimataifa. Tuna imani watakaopanda watafurahi, lengo ni kuona hata aliye na usafiri wake binafsi anauacha nyumbani na kutumia huu,” amesema.

Kassim amesema kutokana na kufungwa mifumo ya kisasa, wana imani abiria hatakaa zaidi ya dakika tatu hadi tano kituoni kusubiri gari.

Zubeda Kimweri, mkazi wa Mbagala, amesema wanaona kuna mwanga wa kuanza huduma ya usafiri baada ya kuyaona mabasi kwa macho kwa kuwa ahadi zilikuwa zikitolewa mara kwa mara bila utekelezaji.

Daudi Njau, mkazi wa Chamazi, ameshauri waendeshaji wa mabasi hayo wahakikishe yanaingia barabarani mara moja.

“Kuyaleta mabasi ni suala moja na kuyaingiza barabarani ni jingine, maana tulishashuhudia haya kwa yale mabasi 70 wakati ule, yaliyokaa muda mrefu bila kutumiwa. Tukumbuke hivyo vyombo vya moto visipotumiwa vinaharibika,” amesema.

Mabasi hayo yenye urefu wa mita 18 yana uwezo wa kubeba abiria 160 kila moja.

Kwa mujibu wa Kassim, huduma itakapoanza abiria 325,000 hadi 400,000 wanatarajiwa kusafirishwa kwa siku.