Banjul. Wizara ya Mambo ya Nje nchini Gambia, imetoa taarifa ya vifo vya watu 70 baada ya kupinduka kwa mashua waliokuwa wakisafiria.
Imeelezwa kuwa, ajali hiyo imetokea baada ya abiria wa mashua hiyo kusogea upande mmoja wa mashua walipoona mwanga wa mji wa Mheijrat, karibu kilomita 80 kaskazini mwa mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Reuters mashua hiyo imepinduka ikiwa ikiwa na abiria 160, wengi wakiwa ni raia wa Gambia na Senegal.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Gambia imesema tukio hili ni ajali mbaya zaidi kuwahi kutokea katika pwani ya Taifa hilo na kuwataka raia wa Gambia wenye lengo la kusafiri kwa kutumia njia hii kuacha mara moja ili kunusuru maisha yao.
“Tunawasihi raia wetu kujiepusha na safari hizo hatari, ambazo zinaendelea kupoteza maisha ya wengi,” imesema taarifa ya wizara.
Hili ni moja ya matukio miongoni mwa mengi ya ajali za vyombo vya majini katika maeneo hayo na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM), takriban watu 8,938 walikufa mnamo 2024 wakijaribu kuvuka mipaka wa njia hatari ya baharini kati ya Afrika na Ulaya.
Watu wengi wanaosafiri kwenye Ulaya kupitia Mauritania wakitokea nchi jirani za Senegal na Mali, hukumbana na kadhia kama hizi kutokana na mikondo ya bahari yenye nguvu na hali tete ya vyombo.