Chamwino. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameahidi kumaliza changamoto zote za huduma za kijamii katika Jimbo la Chamwino kwa kile alichoeleza kuwa “Jimbo la Rais halitakiwi kuwa na changamoto zozote.”
Samia ametoa ahadi hizo leo Jumapili, Agosti 31, 2025, Chamwino mkoani Dodoma, ikiwa ni kituo chake cha kwanza cha kampeni katika siku ya leo, huku akitarajiwa kufanya mikutano mingine katika majimbo ya Chemba, Kondoa na Dodoma mjini.
Akiwa Chamwino, Samia amewashukuru majirani zake, jimbo ambalo kuna Ikulu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, huku akiwaahidi makubwa akichaguliwa kuendelea kuiongoza Serikali.

Mgombea huyo amesema mengi yamefanyika katika jimbo hilo, lakini anatambua bado kuna mengi yanayohitaji kufanyika kwa kuwa Chamwino ni nyumbani kwa Rais.
“Tutakuja kuongeza vituo vya afya 10 na zahanati tano katika jimbo hili la Chamwino. Jimbo la Rais halitakiwi kuwa na changamoto zozote,” ameahidi mgombea huyo.
Ameongeza kuwa atahakikisha kwamba Chamwino yote inapata maji na pia watajenga kilomita 10 za barabara kwa kiwango cha lami, na kuhakikisha maeneo mengine yanapitika.
“Tutapeleka barabara za changarawe katika maeneo yenye uhitaji, barabara za kupitika wakati wote. Pengine hatutaanza na lami, lakini tutahakikisha zinapitika wakati wote,” amesema.
Kwa upande wa kilimo, amesema wanakwenda kuanzisha mashamba makubwa Chamwino, kama yale ya Chinangali, ili wapate mahali pa kuwawekea vijana ili wazalishe.

Awali, akizungumza kwenye mkutano huo, mgombea ubunge wa CCM Jimbo la Chamwino, Deo Ndejembi, amebainisha mafanikio katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye sekta za elimu na afya.
“Mradi mkubwa wa maji bado unaendelea. Ukikamilika utaleta maji ya uhakika hapa Chamwino. Tulikuwa na changamoto ya daraja katika kata ya Nzari, ulituletea Sh14.5 bilioni kwa ajili ya kujenga daraja hilo. Sasa panapitika vizuri,” amesema Ndejembi.
Mgombea huyo ameomba jimbo hilo liwe na halmashauri yake ili kurahisisha shughuli za kiutawala, kwani jiografia yake inawasumbua wananchi wake.
Hata hivyo, akizungumzia ombi hilo, Samia amesema wamepokea ombi hilo, licha ya kwamba mkakati wa Serikali si kuongeza halmashauri nyingine, bali kuziimarisha zilizopo.
“Niseme tu kwamba tumelipokea. Tutaliangalia kama kuna uhitaji wa kuwa na halmashauri ya Chamwino,” amesema mgombea huyo wa urais kupitia CCM, ambaye pia anatetea nafasi hiyo.