MABAO mawili yaliyofungwa na Joseph Akadwanaho na Ramadhan Chobwedo, yametosha kuipa furaha Tabora United na kupeleka kilio Fountain Gate.
Hiyo ilikuwa katika mchezo wa kwanza wa Kundi A kwenye michuano ya Tanzanite Pre-Season International iliyoanza leo Agosti 31, 2025.
Michuano hiyo inayofanyika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manywara, Akandwanaho alianza kuifungia Tabora United dakika ya 6 kwa mkwaju wa penalti.
Mkwaju huo ulitokana na beki wa kati wa Fountain Gate, Antony Nwadioha kumchezea vibaya mshambuliaji wa Tabora United, Adam Omary Adam.
Akandwanaho alikuwa mwiba mchungu kwa Fountain Gate kwani dakika ya 27 akatoa pasi safi kwa Ramadhan Chobwedo aliyeiandikia Tabora United bao la pili.
Kuingia kwa mabao hayo yaliyopatikana ndani ya dakika 30 za kwanza, iliifanya Fountain Gate kujiuliza inakwama wapi, lakini haikupata majibu na kujikuta ikienda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, mabadiliko yaliyofanywa na makocha wa timu zote, Denis Kitambi wa Fountain Gate na Kaunda Simonda wa Tabora United, hayakubadili ubao zaidi ya kuleta burudani kwa mashabiki kutokana na kandanda safi lililokuwa likicheza muda mwingi katikati ya uwanja.
Mchezo huo uliomalizika kwa Tabora United kushinda mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate, ulikuwa ni wa kundi A, ambalo lina timu nyingine ya Bandari kutoka Kenya.
Mashindano ya Tanzanite Pre-Season International yanafanyika kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa uliopo Babati mkoani Manyara, yameanza leo Agosti 31, 2025 na tamati yake ni Septemba 7, 2025, yakiandaliwa na Fountain Gate FC.
Jumla ya timu 10 zinashiriki zikiwa zimepangwa katika makundi matatu. Mbali na Kundi A lenye timu tatu, Kundi B zipo Tanzania Prisons, Dodoma Jiji na Coastal Union zote za Tanzania Bara huku Kundi C kuna Namungo kutoka Tanzania Bara, JKU ya Zanzibar, City Abuja (Nigeria) na TDS inayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kesho Jumatatu Septemba 1, 2025, michuano hiyo itaendelea ambapo JKU itapambana na TDS saa 7:00 mchana kisha City FC Abuja ikicheza dhidi ya Namungo saa 10:00 jioni.