Aliyekuwa Spika Bunge la Ukraine auawa kwa kupigwa risasi

Dar es Salaam. Aliyekuwa Spika wa Bunge la Ukraine, Andriy Parubiy ameuawa kwa kupigwa risasi katika Jiji la Magharibi la Lviv jana Jumamosi, kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu.

Taarifa zinaeleza kuwa,  mtu mwenye silaha alifyatua risasi kadhaa na kumuua Parubiy papo hapo kisha kukimbia na msako mkubwa umeanzishwa kumtafuta muuaji huyo.

Parubiy (54), alikuwa mbunge na alihudumu kama Spika wa Bunge kuanzia Aprili 2016 hadi Agosti 2019. Pia alikuwa mmoja wa viongozi wa maandamano ya Euromaidan ya mwaka 2013–2014 yaliyokuwa yakipigania uhusiano wa karibu zaidi kati ya Ukraine na Umoja wa Ulaya.

Aidha, alihudumu kama Katibu wa Baraza la Usalama na Ulinzi la Taifa (NSDC) kuanzia Februari hadi Agosti 2014, kipindi ambacho mapigano mashariki mwa Ukraine yalianza na Russia iliponyakua Rasi ya Crimea, kwa mujibu wa Citizen Digital ya Kenya.

Rais Volodymyr Zelenskiy amethibitisha mauaji hayo kupitia X (zamani Twitter), akitoa pole kwa familia na kuahidi vyombo vyote vya usalama vimehusishwa katika uchunguzi na msako wa mtuhumiwa.

Polisi walisema tukio hilo lilitokea saa sita mchana kwa saa za Lviv. Meya wa jiji hilo, Andriy Sadovyi amesema kumtambua muuaji na kubaini mazingira ya shambulio hilo ni jambo la kipaumbele, akisisitiza kuwa ni suala la usalama wa taifa wakati wa vita.

Kufuatia mauaji hayo viongozi na wanasiasa mbalimbali wametoa salamu za rambirambi akiwemo Rais wa zamani Petro Poroshenko alisema mauaji hayo ni ya risasi iliyopigwa kwenye ‘moyo wa Ukraine’ na kumtaja Parubiy kama rafiki wa kweli na mjenzi wa Jeshi la Ukraine.

Waziri Mkuu Yulia Svyrydenko amelitaja tukio hilo kuwa ni pigo kubwa na kutoa wito wa uchunguzi wa haraka.

Akinukuliwa na RFI, Rais Zelenskyy amesema, “Kwa bahati mbaya, uhalifu huo ulipangwa kwa uangalifu mkubwa.”