STRAIKA wa zamani wa TP Mazembe, Simba na Yanga, Jean Baleke ametua Rayon Sports ya Rwanda kwa kupewa mwaka mmoja wa kuitumikia klabu hiyo iliyomaliza nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Rwanda msimu uliopita ikizidiwa pointi nne na mabingwa mara sita mfululizo, APR.
Nyota huyo raia wa DR Congo kwa muda wa miezi sita hakuwa na timu baada ya kukatishiwa mkataba na Yanga aliojiunga nayo mwanzoni mwa msimu uliopita na kutemwa katika dirisha dogo, anakumbukwa na mashabiki wa Simba kutokana na kuifungia mabao muhimu alipokuwa na kikosi hicho.
Baleke aliyetua Msimbazi kwa mkopo kutoka TP Mazembe ya DR Congo Januari mwaka 2023 kupitia dirisha dogo na kuifungia mabao manane kabla ya kuongeza mengine manane msimu uliofuata na kurudishwa TP Mazembe na baadae kupelekwa Al Ittihad ya Libya kabla ya Januari 8, mwaka jana kujua Yanga ambapo aliifungia bao moja tu la Ligi kabla ya kutemwa.
Awali ilikuwa ikielezwa alikuwa mbioni kutua AmaZulu ya Afrika Kusini na baadae kuhusishwa na Namungo, lakini dili zote zilikwama na juzi kati ndipo alipotambulishwa na Rayaon Sports iliyotoka kucheza mechi ya kirafiki ya kimataifa na Yanga na kucharazwa mabao 3-1 katika Tamasha la Rayon lililofanyika katikati ya mwezi huu wa Agosti.
Kutua kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 24 aliyewahi kucheza soka la kulipwa Lebanon kunaweza kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji wa Rayon inayohaha kusaka ubingwa wa Ligi Kuu ya Rwanda tangu ilipotwaa mara ya mwisho msimu wa 2018-2019 kutokana na APR kutawala ligi hiyo ikitwaa ubingwa mara sita mfululizo sasa.
Klabu hiyo ya Rayon pia imemtambulisha straika mwingine kutoka Burundi, Asman Ndikumana aliyepewa mkataba wa miaka miwili na kumfanya Baleke awe na kibarua cha kuchuana na Mrundi huyo kuweza kupata namba mbele ya kocha Afhamia Lotfi raia wa Tunisia aliyetua Mei mwaka huu akitokea Mukura Victory.
Rayon Sports itaiwakilisha Rwanda katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ikianza kibarua chao dhidi ya Singida Black Stars ya Tanzania mechi zitakazopigwa kati ya Septemba 19-28, Wanyarwanda hao wakianzia nyumbani na kumalizia ugenini, jijini Dar es Salaam.