Kondoa. Chama cha Mapinduzi (CCM), kimeahidi kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo cha kisasa katika eneo la Pahi lililopo Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.
Mashamba hayo yatawekewa skimu za umwagiliaji ili kuwawezesha wakulima kulima mara mbili kwa mwaka, jambo litakalochochea uzalishaji mkubwa na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Hayo yamebainishwa na mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan, leo Jumpili Agosti 31, 2025 wakati wa kampeni zake katika Jimbo la Kondoa, alikopata mapokezi makubwa ya wananchi.

Samia ameahidi mambo mbalimbali kwa wananchi hao, ikiwamo kutengeneza mazingira mazuri kwa wakulima wa Kondoa ili waongeze uzalishaji na kunufaika na kilimo chao.
“Tunakwenda kuanzisha mashamba makubwa ya kilimo cha kisasa katika maeneo ya Pahi. Vilevile, tutatekekeza mradi wa skimu za umwagiliaji kule Beleko, hekta 150, ili wakulima waweze kulima mara mbili kwa mwaka,” ameahidi mgombea huyo.
Pia, amesema kuboresha mazingira ya biashara huko Pahi na kujenga soko kubwa huko Bukuli ili wakulima wapate soko la uhakika kwa mazao wanayozalisha.
Samia amesema wanakwenda kujenga daraja la Bukuli na pia wataboresha barabara za Kondoa Vijijini ili zipitike wakati wote.
Amewataka wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo wajitokeze kumpigia kura yeye pamoja na wagombea ubunge, Dk Ashatu Kijaji (Kondoa) na Mariam Ditopile (Kondoa Mjini), na madiwani wote wa CCM.
Dk Bashiru aibukia Kondoa
Katika mkutano wa kampeni Jimbo la Kondoa Mjini, Katibu Mkuu wa zamani wa CCM, Dk Bashiru Ally amepewa nafasi ya kusalimia wananchi waliojitokeza katika mkutano huo huku akisema Kondoa ni ukweni kwake, hivyo amekwenda kumwombea kura Dk Kijaji na kutekeleza maelekezo ya Mwenyekiti, Rais Samia, ya kukitafutia kura chama hicho.
Amempongeza Samia kwa kusimamia umoja na mshikamano ndani ya CCM na Taifa kwa jumla. Amesisitiza kwamba, nguvu ya CCM inatokana na nguvu ya umoja huo.
“Nakupongeza sana ndugu mwenyekiti, umeisimamia vizuri kazi ya kukiunganisha chama, umeisimamia vizuri kazi ya kuliunganisha Taifa,” amesema Dk Bashiru huku akiwaombea kura wagombea wa CCM.
“Nchi yetu inafanya vizuri katika maeneo mengi. Tuko hapa kukinadi chama chetu kwa ubora wake, tunaomba muendelee kumwamini… Samia, muendelee kukiamini Chama cha Mapinduzi,” amesema Dk Bashiru.
Awali, Dk Kijaji ameeleza mafanikio makubwa yaliyopatikana katika jimbo lake wakati akiwa mbunge huku akiwaomba wananchi wampigie kura ili akamalizie mambo mengine yaliyosalia kwa ajili ya maendeleo yao.
Amesema wakati Samia anaingia madarakani, Kondoa ilikuwa na visima viwili pekee vya maji safi, lakini sasa wana visima 154 huku miradi mingine ya maji ikiendelea katika wilaya hiyo.
“Wakati unaingia madarakani, hatukuwa na kituo cha afya, lakini sasa tuna vituo sita, kikiwamo kimoja ulichotukabidhi hivi karibuni,” amesema mgombea huyo.
Kwa upande wa sekta ya nishati, Dk Kijaji amesema vijiji 84 na vitongoji 300 katika wilaya ya Kondoa, havikuwa na umeme kabisa, lakini sasa vijiji vyote vina umeme huku vitongoji 221 vikiwa vimefikiwa na huduma hiyo, hivyo vimebaki vichache ambacho wanakwenda kuvikamilisha katika miaka mitano ijayo.