CHAN ilivyoisha na utamu wake

ACHANA na matokeo ya fainali ya mashindano ya CHAN 2024 iliyopigwa jana kati ya Morocco na Madagascar, lakini kipute hicho kilichoanza Agosti 2 – 30, 2025 kwa mara ya kwanza kilihusisha nchi tatu wenyeji ikiwa ni Kenya, Tanzania na Uganda, lakini kimeweka historia mpya kwa kuvunja rekodi mbalimbali.

Hii ilikuwa ni hatua kubwa katika kukuza hadhi ya mashindano ya wachezaji wa ligi za ndani Afrika.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilitangaza ongezeko kubwa la zawadi kwa bingwa, ambapo timu iliyotwaa ubingwa jana, Jumamosi ilijipatia Dola 3.5 milioni sawa na ongezeko la asilimia 75 kutoka Dola 2 milioni zilizotolewa mashindano yaliyopita. Ongezeko hilo liliifanya CHAN 2024 kuwa na jumla ya zawadi za Dola 10.4 milioni sawa na ongezeko la asilimia 32.

Mgawanyo wa zawadi nao ulikuwa si mchezo. Mbali na bingwa kupata Dola 3.5 milioni, mshindi wa pili Dola 1.2 milioni, nafasi ya tatu ambao ni Senegal imelamba Dola 700,000 huku ya nne Sudan ikiondoka na Dola 600,000.

Timu zilizofika robo fainali ikiwemo wenyeji wa michuano zimeondoka na Dola 450,000 kila moja, ilhali zilizoshiriki na kuishia hatua ya makundi kama Nigeria ambayo ilikuwa ya kwanza kuaga zilipewa kati ya Dola 200,000 hadi 300,000, jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya mashindano hayo.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa CAF kutoa zawadi kwa timu zote zilizoshiriki bila kujali hatua waliyofikia. Hapo awali, ni timu bora pekee ndizo zilizokuwa zikifaidika na mgao wa fedha.

Hatua hii imeweka misingi mipya ya usawa na kuongeza hamasa ya ushindani kwa kila mshiriki.

Mashi-ndano haya pia yalihusisha mageuzi ya teknolojia. Kwa mara ya kwanza, mfumo wa VAR wa kidigitali ulitumika kwa upana katika mechi zote, huku wanawake wakipewa nafasi katika majukumu ya uamuzi wa michezo. Hili lilionekana kama hatua ya wazi kuelekea kuimarisha usawa wa kijinsia kwenye soka la Afrika.

Uwanjani, rekodi kadhaa ziliwekwa ikiwemo wenyeji wote kwa pamoja kutinga robo fainali haijawahi kutokea kwa wenyeji kufanya hivyo kwenye mashindano ya CAF. Sudan nayo iliandika historia kwa kuilaza Nigeria mabao 4-0, matokeo ambayo yalizua mijadala na kustua.

Mashindano ya mwaka huu pia yalikuwa ya kwanza kuandaliwa na mataifa matatu kwa pamoja, yakionyesha mshikamano wa kikanda na kuimarisha ushirikiano wa miundombinu ya michezo Afrika Mashariki. 

CAF ilieleza kuwa ongezeko la zawadi ni sehemu ya mkakati wa kuwekeza katika soka la ndani, kuwapa wachezaji motisha ya kuonyesha vipaji vyao na kuifanya CHAN kuwa mashindano ya kukuza nyota wapya.  Wadhamini na mashirika ya matangazo pia waliongeza uwekezaji kutokana na hadhi mpya ya mashindano.

Kwa kulinganisha na 2014 bingwa wa CHAN alipata Dola 750,000, huku jumla ya zawadi ikiwa Dola 3.25 milioni. Tofauti hiyo inaonyesha hatua kubwa iliyopigwa ndani ya kipindi cha muongo mmoja, huku CAF ikielekeza nguvu kwenye thamani ya mashindano. Ushirikiano wa mataifa matatu, ongezeko la zawadi, teknolojia ya VAR, nafasi kwa wanawake na rekodi za uwanjani vimefanya CHAN kunoga huku mtihani ukibaki kwa wenyeji kujipanga na mashindano ya Afcon 2027.