Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) leo, tarehe 31 Agosti 2025, kinatarajia kuzindua rasmi kampeni za mgombea wake wa urais, Salum Mwalimu, pamoja na mgombea mwenza wake Devotha Minja, jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Habari na Taarifa kwa Umma wa CHAUMMA, John Mrema, uzinduzi huo utafanyika katika Viwanja vya Kinondoni Biafra, badala ya Temeke kama ilivyokuwa imeelezwa awali.
Kwa upande mwingine, Chama cha Wananchi (CUF) nacho leo kinazindua kampeni zake katika Uwanja wa Furahisha, Ilemela – Mwanza, kupitia mgombea wake wa urais, Samandito Gombo, ambaye amesema uamuzi wa kuanzia Mwanza unatokana na nafasi ya mkoa huo kisiasa na pia kuwa nyumbani kwake.
“Mwanza ni nyumbani kwetu, mimi si mgeni. Tumeamua kufungua kampeni hapa kwa sababu huu ni mkoa wa kimkakati kwa chama chetu katika safari ya kuingia Ikulu,” alisema Gombo.
Aidha, chama cha AAFP pia kimepangwa kuzindua kampeni zake leo mkoani Morogoro chini ya mgombea wake wa urais Kunje Ngombare Mwiru, akishirikiana na mgombea mwenza Chumu Abdallah Juma.
Kwa mujibu wa ratiba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), vyama vya siasa vilianza rasmi kampeni tarehe 28 Agosti 2025. Hata hivyo, vyama vya ADC na NRA vilivyotarajiwa kuanza siku hiyo, viliahirisha.
ADC imesema inasubiri uamuzi wa pingamizi dhidi ya mgombea wake, na sasa imepanga kuzindua kampeni 7 Septemba 2025.
NRA kwa upande wake ilieleza kuwa ratiba ngumu ilisababisha mgombea wake wa urais, Hassan Kisabya, kukwama njiani kuelekea Kigoma na kulazimika kurejea Dar es Salaam kwa maandalizi mapya.
Ikumbukwe kuwa chama tawala CCM ndicho kilichoongoza kuzindua kampeni zake tarehe 28 Agosti 2025, kupitia mgombea wake ambaye pia ni Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan, katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam.
Wakati huohuo, jana chama cha CCK kilizindua rasmi kampeni zake jijini Dar es Salaam kupitia mgombea wake wa urais David Daud Mwaijojele, akishirikiana na mgombea mwenza Masoud Ali Abdala, katika viwanja vya Mtoni Kijichi.