Moshi. Mchakato wa kuandika Katiba mpya unaonekana kuwa moja ya turufu katika uchaguzi mkuu 2025 huku Chama cha Wananchi (CUF), kikiahidi kuanza na rasimu ya Jaji Joseph Warioba na Katiba Inayopendekezwa.
Karibu vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 29,2025, vimetoa ilani ya maandishi, suala la kufufua mchakato wa Katiba mpya ni moja ya ajenda zilizopewa kipaumbele na vyama hivyo.
Mchakato wa kuandika Katiba mpya ulikwama mwaka 2014 baada ya Bunge Maalumu la Katiba chini ya uenyekiti wa Samwel Sitta, kupitisha Katiba Inayopendekezwa, iliyopaswa kwenda kupigiwa kura ya Ndiyo au Hapana.
Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Nne haikuweza kuipeleka Katiba katika hatua ya upigaji kura kutokana na muda na Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani chini ya John Magufuli, ikisema Katiba mpya sio kupaumbele chake.
Ilani hiyo ya CUF, imewaibua wachambuzi wa siasa na wasomi wakiwamo mawakili, licha ya kuipongeza CUF kwa ahadi hizo, baadhi walitilia shaka mfumo wa sasa wa uchaguzi kama utawawezesha kushika dola.
Kupitia ilani yake ya uchaguzi, CUF inaeleza kuwa, utaratibu wa kupata Katiba mpya utaanza na uchambuzi wa Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na Katiba Inayopendekezwa ya Bunge la Katiba na hili litafanyika ndani ya miezi mitatu.

Serikali ya Umoja wa Kitaifa
CUF kupitia ilani hiyo, inasema Tanzania kwa sasa imejaa ufisadi, ubinafsi, mgawanyiko, kuumizana, ubaguzi na watu kutekwa na kuuana; majeraha yanayohitaji kutibiwa na kuwarejeshea wananchi matumaini.
“Tumefikia hapa tulipo kutokana na Tanzania kukosa taasisi imara za kusimamia uendeshaji wake. Taasisi zilizopo uimara wake ni wa kinadharia kuliko wa uhalisia. CUF inataka nchi iwe na taasisi imara bila kujali chama gani kipo madarakani.
“Kuunda mfumo huu kunahitaji nguvu ya pamoja na ushirikishwaji wa kila Mtanzania. Kwa sababu hii, CUF inapendekeza Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Serikali hii jumuishi itakuwa na jukumu la kujenga mfumo unaohitajika,”inaeleza.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya CUF itaweka misingi ya kuhakikisha Taifa linakuwa na Demokrasia ya kweli. Serikali itakamilisha mchakato wa kupata Katiba mpya yenye misingi imara ya demokrasia na utawala bora,”inasisitiza CUF.
CUF kupitia ilani yake hiyo, inasema inahitajika Katiba ambayo, pamoja na mambo mengine, itatenganisha mamlaka na nguvu za mihimili ya dola, italinda misingi ya ushindani wa kisiasa, itapanua na kukuza haki za kiraia, na itahakikisha uwepo wa uhuru wa kutosha wa vyombo vya habari na fursa ya kujieleza.
“Tunahitaji kuwa na Katiba nzuri inayompa kila Mtanzania uhuru wa kweli wa kuchagua na wa kuchaguliwa. Tunahitaji kuwa na Muungano wa Watanganyika na Wazanzibari usio na shaka ndani yake kwa pande zote mbili,”inaeleza.
“Kuna Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge la Katiba. Utaratibu wa kupata Katiba mpya utaanza na uchambuzi wa Rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba na Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge Maalumu la Katiba.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya CUF itahakikisha kuwa, mchakato wa uandaaji wa Katiba mpya ya wananchi utafufuliwa katika kipindi cha miezi mitatu baada ya Serikali kuapishwa,” kinaeleza chama hicho katika ilani hiyo.

Kwa mujibu wa ilani hiyo, Katiba ya wananchi itaandaliwa kwa kushirikisha wadau wote katika mjadala wa kitaifa, ikiwa ni pamoja na wataalamu wa katiba, Vyama vya siasa, madhehebu ya dini, wakulima, vijana, wakulima na wafanyakazi.
“Mjadala huu utajikita katika kuboresha Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Warioba,” inasema ilani hiyo na kuongeza kuwa maoni yatakayokusanywa katika mjadala huo ndiyo yatakuwa msingi mkuu wa kuandaa Rasimu ya Katiba mpya.
“Katiba mpya itapatikana katika kipindi cha Bunge la mwaka mwaka wa fedha 2026/27 na uchaguzi wa Serikali za mitaa wa mwaka 2028 na uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2030 utafanyika nchini tukiwa na Katiba Mpya,”inaeleza.
CUF kupitia ilani hiyo, inasema Katiba mpya itabainisha wazi kuwa makubaliano ya Muungano ya mwaka 1964 ndiyo sheria mama ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania ambayo kimantiki yanataka uwepo wa muundo wa Serikali tayu.
Katika ilani hiyo, Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya CUF itafuta sheria zote kandamizi na kuhakikisha haki za kila raia zinalindwa.
“Kupitia Katiba ya wananchi, Serikali ya Umoja wa Kitaifa chini ya CUF itaweka mazingira ya kuheshimu kikamilifu utawala wa sheria na ulinzi wa haki za binadamu na itafuata Katiba na sheria katika utekelezaji wa majukumu yake,”inaeleza.
Halikadhalika CUF imeahidi kuwa, Serikali yake itaweka saini na kuridhia Mkataba wa Afrika wa Demokrasia, Uchaguzi na Utawala Bora unaozitaka nchi za Kiafrika kuheshimu misingi ya demokrasia ya kweli, kufanya uchaguzi ulio huru na wa haki.
Pia, mkataba unataka kuongoza nchi kwa kufuata kanuni za utawala bora na kwamba mpaka sasa Serikali CCM imekataa kutia saini na kuridhia mkataba huu.
CUF inasema Umoja wa Kitaifa utaweka saini na kuridhia Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa mwaka 1984 dhidi ya utesaji na adhabu nyingine za kikatili zisizo za kibinadamu zinazodhalilisha na kwamba hadi sasa Serikali haijauridhia.

Akizungumzia ilani hiyo ya CUF, Wakili David Shillatu anasema: “Kuhusu Katiba mpya nadhani CUF ilipaswa ijielekeze kwenye maoni kama yalivyokua katika tume ya Jaji Warioba, maoni yaliyomo katika Tume ya Warioba ni maoni ya Wananchi na maoni hayo yanaishi hadi leo.
“Kuhusu Tanzania kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa juu ya haki za binadamu ni jambo jema kwa kuwa, Tanzania haiwezi kuishi kama kisiwa, lakini haya yote yawezekana kama kutakuwa na Katiba mpya yenye meno.
“Ni lazima tuwe na Katiba yenye meno itakayowajibisha ipasavyo mifumo yote ya kiutendaji katika zile nguzo tatu za dola kwa maana ya Bunge, Mahakama na Serikali yenyewe. Bila hivyo ni kutwanga maji kwenye kinu,”anasisitiza.
Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii kutoka Bukoba, Cyprian Mgema anasema ahadi za CUF ni nzuri na zinavutia, lakini anachokiona kuna tatizo kubwa la mifumo na sheria za uchaguzi zinazotoa haki kwa wagombea.
“Ukizisoma ni ahadi nzuri kwa kweli, swali ni mifumo ipi ya uchaguzi itakayowaruhusu kushika dola? Ni kweli tunahitaji Katiba mpya na yote wanayoyasema hata sheria kandamizi zifutiliwe mbali lakini watatoboa?”anahoji Mgema.
Kwa upande wake, Wakili Peter Mshikiliwa anasema mapendekezo ya CUF yamebeba matumaini hasa suala la Katiba mpya kwa kuwa, yaliyopo yanashindwa kutoa suluhisho la kero ya Muungano na kutibu changamoto zinazoikabili nchi.
Wakili Stephen Mduma anasema: “Ni hatua nzuri kwa chama ila sidhani kama vipaumbele hivyo vinaakisi uhalisia wa mashindano ya kisiasa yanayoendelea kwani CUF imepoteza ile nguvu ya upinzani iliyokuwa nayo.
“Ingawa vipaumbele hivyo ni hatua kubwa kwa chama, lakini nina wasiwasi kama watapata ushawishi wa wananchi kwa kipindi hiki cha uchaguzi wa mwaka huu,”anasema wakili Mdume.