CUF yataja mwarobaini wa wizi mali za umma

Mwanza. Chama cha Wananchi (CUF) kimefungua rasmi kampeni zake za kuomba kura kwa wananchi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu, huku kikisema, wezi wote wa mali za umma hawatafungwa jela isipokiwa watatakiwa kurejesha mali.

‎Ufunguzi huo umefanyika leo Jumapili Agosti 31, 2025 katika Uwanja wa Furahisha wilayani Ilemela Mkoa wa Mwanza ukihudhuriwa na mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

‎Baada ya kuzindua kampeni zake jijini Mwanza, chama hicho kesho Jumatatu, Septemba mosi, 2025 kitafanya kampeni wilayani Bunda Mkoa wa Mara.

‎‎Akinadi sera za chama hicho, mgombea urais Gombo Samandito Gombo amesema katika utawala wake, wezi wote wa mali za umma hawatafungwa jela isipokiwa watatakiwa kurejesha mali walizoiba na wasipofanya hivyo watafilisiwa.

‎Gombo amesisitiza kuwa, wananchi ndiyo watakuwa waamuzi wa mwisho wa adhabu gani zitawafaa wezi hao, chochote kitakachoamuliwa na wananchi kitatekelezwa na Serikali ya CUF.

‎”Katika kudhibiti suala la wizi kwa watumishi wa umma, tutafanya mambo yafuatayo; mtumishi wa umma akiiba mali ya umma atarudisha fedha aliyoiba, hatuna sababu ya kumpeleka jela, sisi tunataka fedha zetu, kama hana tutamfilisi,” amesema Gombo.

‎‎ “Akishatulipa tunamuachia aende zake, hatuna haja ya kujaza magereza, na hataruhusiwa tena kufanya kazi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, vyeti vyake tutachoma na tunamfukuza kazi. Kama wewe unafikiri utaiba basi acha kuajiriwa kwa sababu haya yatakukuta,”amesema Gombo.

‎Mgombea huyo amesema miongoni mwa mambo ya kwanza watakayoyafanya ni kuboresha Katiba na kuandaa katiba mpya baada tu ya kuapishwa.

‎Mbali na Katiba mpya, Gombo amesema chama hicho kitahakikisha Serikali inakuwa na ‘satellite’ yake kuhakikisha huduma za mawasiliano zinakuwa huru na gharama nafuu.

“Nasema haya mniamini najua Serikali yetu ina fedha, msione kama naongea maneno matupu najua tuna rasilimali za kutosha na fedha inakoweza kupatikana kwa sababu nimekuwa mtumishi wa umma nafahamu vizuri,” amesema Gombo.

Awali,  akimnadi mgombea urais wa CUF, mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba amesema chama hicho kimemteua mgombea urais thabiti ambaye ni kiboko na atakitetemesha Chama cha Mapinduzi (CCM).

‎Mbali na Gombo, mgombea mwenza wa chama hicho ni Husna Mohamed Abdallah.

‎‎Profesa Lipumba amesema wagombea hao wanazijua shida za Watanzania na wanataka kuhakikisha wananchi wanapata hali sawa na rasilimali za nchi zinanufaisha Watanzania wote.

‎”CCM wataanza kupata joto kwamba, CUF wanatuletea mgombea thabiti mwenye uwezo wa kupambana. Nchi yetu iko njia panda ufisadi na rushwa vimekithiri,” amesema Profesa Lipumba.

‎Amesema chama hicho kilimshauri Serikali  kupambana na rushwa na ufisadi lakini ushauri wao ukatupwa kapuni, jambo ambalo limesababisha vilio vya wananchi kila kona ya nchi, huku akiahidi kwamba CUF itapambana na rushwa na ufisadi ambao umekithiri nchini.

‎”Ndugu zangu CCM hawafai, tunawaletea mgombea ameshashika jembe kwenda kulima, ameshachunga ng’ombe, ameshavua samaki. Mgombea wetu anajua matatizo ya Watanzania wa kawaida,” amesema mwenyekiti huyo.

‎ “CCM haizungumzii utawala bora wala kupambana na ufisadi, tunawaletea mgombea atakayepambana kuleta maisha bora.”

‎Akimzungumzia mgombea mwenza, Husna ambaye hakufika uwanjani hapo kutokana na dharura, Profesa Lipumba amesema: “Tunaye mgombea mwenza, Bi Husna yeye ni mwalimu kwa taaluma, ana msimamo thabiti wa kuitetea Tanzania, anajua matatizo yanayotukabili.”

‎”Kwa hiyo tunawaletea timu ambayo itafanya kazi pamoja kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha Watanzania wote,” amesisitiza Profesa Lipumba.