RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambaye pia ni Mgombea Mteule wa Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), amechukua fomu ya kugombea nafasi hiyo katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na kuahidi kuwa CCM itafanya kampeni za kistaarabu zitakazozingatia Utamaduni, Silka na Desturi za Wazanzibari.
Dkt. Mwinyi amechukua fomu hiyo katika Afisi za Tume ya Uchaguzi leo, tarehe 30 Agosti 2025, asubuhi, na hatimaye msafara wake ukaelekea Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui kupitia Barabara ya Miembeni, Kariakoo, Rahaleo na Michenzani, akisindikizwa na mamia ya wanachama wa chama hicho waliokuwa wamejipanga pembezoni mwa barabara.
Aidha, Dkt. Mwinyi amezuru Kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume, na kisha kuzungumza na Wazee wa Chama Cha Mapinduzi afisini hapo.
Akizungumza na mamia ya wanachama wa CCM katika Uwanja wa Mao Tse Tung, Mgombea Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesisitiza kuwa CCM itafanya kampeni zitakazoepuka chuki, mifarakano na ubaguzi miongoni mwa wananchi, na badala yake kufanya kampeni zitakazowaunganisha Wazanzibari kwa kuzingatia maslahi yao ya kijamii na kiuchumi.
Ameeleza kuwa katika kampeni hizo, CCM itaonesha mafanikio yaliyopatikana katika awamu ya kwanza ya Uongozi wa Awamu ya Nane pamoja na utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2025–2030, ambayo itawasilishwa kwa wananchi wakati wa kampeni.
Aidha, ametoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuungana na kuwapigia kura wagombea wote walioteuliwa na chama hicho katika nafasi zote kuanzia Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani ili kuhakikisha CCM inaendelea kushika dola.
Halikadhalika, Dkt. Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa CCM itaendelea kudumisha hali ya utulivu na amani iliyopo nchini wakati wa kampeni, uchaguzi na baada ya uchaguzi.
.jpeg)
