Tarime. Wakati mgombea mwenza wa urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi akiwaahidi mambo mbalimbali wananchi wa Nyamongo, Wilaya ya Tarime, viongozi wa chama hicho wamevunja makundi yaliyotokana na ubunge wa Tarime Vijijini.
Dk Nchimbi amesema Serikali ya CCM Itatekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami katika vipande vinne na kupanua zaidi huduma za afya, elimu na maji.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumapili, Agosti 31, 2025 katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu iliyofanyika Nyamongo, Jimbo la Tarime Vijijini, Mkoa wa Mara.

Mgombea mwenza huyo amewaeleza wananchi wa Nyamongo kwamba, ndani ya miaka mitano iliyopita mambo mengi yamefanyika na mitano mingine ijayo itakuwa na kasi yenye kusogeza zaidi huduma za jamii.
Ametaja mafanikio ya miaka mitano iliyopatikana Tarime Vijijini ambako mbunge wake alikuwa Mwita Waitara anayegombea tena, kuwa ni ufanisi wa Hospitali ya Nyamwaga na ujenzi wa vituo vya afya kutoka sita hadi sasa viko 11.
Amesema zahanati zilikuwa 31 sasa ziko 50, vituo vya mama na mtoto kutoka 37 hadi sasa vipo 62, shule za msingi zimetoka 137 hadi 162, za sekondari miaka mitano zilikuwa 38 sasa 54, madarasa yalikuwa 637 sasa 1,043.
“Haya maendeleo hayahitaji miwani, aliyefurahi anaona na wanaochukia nao wanaona,” amesema Dk Nchimbi huku akishangiliwa.

Amesema kile walichokifanya miaka mitano nyuma ikiwamo upatikanaji wa majisafi ilikuwa asilimia 51 lakini sasa ni 73, umeme ilikuwa vijijini 68 tu lakini sasa 88.
Dk Nchimbi amesema miaka mitano ijayo:”Zahanati zitoke 50 hadi 70, anachokisema… (mgombea urais CCM), mgonjwa hatakiwi kutembea umbali mrefu. Vituo vya afya vitoke 11 hadi 20. Majisafi na salama itoke asilimia 73 hadi 95.”
Amesema eneo la barabara za lami litapewa kipaumbele miaka mitano ijayo.
Kuhusu barabara za lami zitakazojengwa kipindi cha miaka mitano ijayo, Dk Nchimbi amezitaja ni Tarime- Mgumu kwa kilomita 87, Mogabiri- Nyamongo (25), Tarime Mobagiri (9.3) na Nyamongo- Mgumu kilomita 45.
“… (Samia) na mimi mwenyewe (Dk Nchimbi), wabunge na madiwani tupo tayari kuwatumikia. Tarehe 29 tuchagueni kwa kura nyingi,” awameomba wananchi.

Katika mkutano huo, makundi yaliyotokana na mbio za kuwania ubunge wa Tarime Vijijini ambao umemalizika kwa kuibuka makundi
baina ya Mwita Waitara aliyekuwa anatetea na wagombea ambao baadhi waliungwa mkono na viongozi.
Kwenye kura za maoni zilizofanyika Agosti 4,2025, Waitara aliongoza baada ya kupata kura 4,504 huku akifuatiwa na Edward Machage aliyepata kura 2,303.
Wagombea wengine ni Nyambari Nyangwine aliyepata kura 1,698, Simon Chacha (967) na Deadatus Waikama kura 116.
Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Daudi Ngicho amesema tayari wamevunja makundi ndani ya chama hicho ikiwamo tofauti baina yake na Waitara.
Ngicho amesema wakati wa mchakato wa kura za maoni kulitokea kutokuelewana hali iliyozua sintofahamu lakini tayari tofauti hizo wamezimaliza na wanachokitafuta kwa sasa ni kura za ushindi kwa chama hicho.
“Niwaambie wale ambao walikuwa wanachukua maneno kwa Waitara na kuleta kwangu na wale waliokuwa wanachukua maneno kutoka kwangu kwenda kwa Waitara, niwaamabie leo mwisho, sisi tumemaliza tofauti zetu, kwa pamoja tunatafuta kura za CCM,” amesema Ngicho.
Amesema ushindi wa Waitara na CCM kwa jumla ni ushindi wake yeye, kama mwenyekiti ameona hakuna sababu ya kuendelea na tofauti zao badala yake waungane pamoja kutafuta ushindi wa CCM.
“Kwa sasa kila mwana CCM jukumu letu ni moja tu ambalo ni kuomba kura, tukatafute kura kwa wananchi tuombe kura kwa unyenyekuvu bila kumtukana mtu yeyote,” amesema.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi amesema amefurahishwa sana na hatua ya mwenyekiti wa wilaya kuvunja makundi ikiwamo tofauti iliyokuwepo kati yake na Waitara.
“Nimefurahi sana leo, hili la kuvunja makundi na kuondoa tofauti kati yetu ndicho kitu nilichokuwa nakitaka, kwakweli mwenyekiti leo nitakuchomea nyama nimefurahi sana,” amesema Chandi.
Amesema kuondoa tofauti hizo ni njia mojawapo ya chama hicho kuelekea kwenye ushindi, huku akitoa wito kwa wana CCM kuwa wamoja katika kutafuta kura kwenye uchaguzi.
Waitara na Ngicho wamekuwa na tofauti kwa muda mrefu hali iliyosababisha chama chao kutafuta suluhu kupitia njia mbalimbali ikiwamo kwa viongozi wa ngazi za juu.
Waitara amemshukuru mwenyekiti wa wilaya kwa kutamka kwamba amevunja makundi.
“Jambo hili limenipa furaha na faraja kubwa sana,” Waitara.
Akiendelea kuzungumza huku sauti ikikwaruza kwaruzwa, amesema hali hiyo (kukwaruza sauti) ni kutokana na furaha aliyo nayo juu ya jambo hilo kumalizwa.
Utofauti huo ulizidi kushika kasi hasa wakati wa kueleka kwenye kura za maoni za chama hicho ilipodaiwa mwenyekiti kumuumga mkono mmoja wa vigogo serikalini ambaye hata hivyo, hakuchukua fomu kuomba ridhaa ya chama hicho.

Katibu wa Oganizesheni wa CCM, Issa Gavu Ussi amesema chama hicho kina tofauti mkubwa na vyama vingine huku akieleza kuwa, sababu ya kwanza ni namna chama chake kimekuwa kikishughulika na matatizo ya wananchi tangu kianzishwe mwaka 1977.
Gavu amesema vyama vingine vimekuwa vikitafuta vyeo na madaraka na kwamba, baada ya uchaguzi huenda likizo na kuwasahau wananchi.
“Sisi ni wa tofauti sana, tangu mwaka 1977 hadi sasa muda wote tunashughulika na wananchi wetu hatujawahi kuwaacha na tunaahidi kuendelea kuwa na wananchi hadi tuifikishe nchi yetu pale tunapopataka yaani kwenye maendeleo makubwa,” amesema Gavu.
Amesema chama hicho kimejitahidi kwa kiwango kikubwa kutatua changamoto za wananchi na kuleta maendeleo huku akisema hali ya Tarime ya sasa katika maendeleo ni tofauti na ilivyokuwa miaka 10 nyuma, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kukiamini chama hicho na kukipa kura za ushindi.
Amesema jukumu kubwa na la msingi la CCM ni kuleta maendeleo na kuharakisha huduma za jamii na kwamba, wananchi waendelee kuwa na imani na chama hicho na kukipigia kura ili imani hiyo iweze kulipwa kwa kuleta maendeleo zaidi kwa masilahi ya wananchi wote.
Kada wa CCM aliyewahi kuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa ameanza kwa kusema:”Tarime si mgeni, nimekuja sana hapa kipindi nikiwa kwa mama wa kambo. Sasa nipo huku sehemu salama.”
Mchungaji Msigwa amesema katika kipindi cha miaka minne ya utawala wa Samia amefanya mambo makubwa na anahitaji kupewa kura nyingi Oktoba 29, 2025 ili aendeleze alipoishia.
“Ukizungumzia barabara, kilimo, afya, umeme na kila sehemu Mama Samia amefanya makubwa kuanzia Newala hadi Mtukura, kuanzia Tarime hadi Kigoma na kwingineko. Sasa kwa nini tusimpe tena mitano aendelee kuyafanya makubwa zaidi,” amesema Mchungaji Msigwa.
Baadaye Dk Nchimbi atafanya mkutano Tarime Mjini na Rorya mkoani Mara.
Endelea kufuatilia Mwananchi