Rorya/Tarime. Mvutano wa kisiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Tarime Mjini limechukua sura mpya baada ya mgombea mwenza wa urais wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi kuumaliza kwa kumteua, Michael Kembaki kuwa kampeni meneja wa Esther Matiko.
Kembaki alikuwa mbunge wa jimbo hilo (2020-2025), katika kura za maoni mwaka huu aliongoza, lakini Halmashauri Kuu ya CCM ikamteua Matiko aliyeshika nafasi ya tatu kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.
Matiko ambaye amewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo (2015-2020) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mwisho wa uhai wa Bunge la 12 akiwa mbunge wa viti maalumu alihamia CCM na kujitosa kwenye mbio za ubunge kupitia chama tawala.
Katika kura za maoni zilizofanyika Agosti 4, 2025, Kembaki aliongoza kwa kupata kura 1,572 akifuatiwa na Jackson Kangoye aliyepata kura 364 na Matiko akishika nafasi ya tatu kwa kupata kura 196 katika kinyang’anyiro hicho kilichoshirikisha wagombea saba.

Tayari Kangoye amejiunga na ACT- Wazalendo na kuteuliwa kugombea ubunge kupitia chama hicho katika Jimbo la Tarime Mjini.
Uamuzi huo wa vikao vya juu kumteua Matiko uliibua maandamano kwa baadhi ya wafuasi wa Kembaki ambao ni wana CCM wakitaka arejeshwe kwani ameongoza kura za maoni na walidai bado anastahili kuwawakilisha na ndiyo maana walimpa kura nyingi kwenye kura za maoni.
Leo Jumapili, Agosti 31, 2025 katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Chuo cha Ualimu Tarime, Dk Nchimbi pamoja na kunadi ilani na kuomba kura, ametangaza uamuzi wa kumaliza makundi na mvutano kwa kumteua Kembaki kuwa meneja kampeni wa Matiko.
Dk Nchimbi amesema uteuzi wa Kembaki kuwa meneja kampeni wa Matiko umebarikiwa na mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan.
Amesema Matiko ana uwezo wa kuwawakilisha vizuri wakazi wa Tarime Mjini na kwamba kati ya wabunge waliomaliza muda wao, Matiko ana uwezo mzuri ana uwezo wa kujenga hoja na muda wote amekuwa akiwasemea na kuwatetea wana Tarime na kuwataka wasiwe na hofu.
Mgombea mwenza huyo amewataka wananchi kuwa na imani na chama hicho kwani kimewateua wagombea wazuri ili kuhakikisha wanakwenda kutekeleza mipango ya Serikali.
Amesema chama hicho kwa kipindi cha miaka mitano imefanya mengi na kuwaomba wananchi kiwape tena ridhaa miaka mitano ijayo.
Dk Nchimbi akihutubia mkutano wa kampeni katika Uwanja wa Mpira, Shirati, Wilaya ya Rorya amebainisha mafanikio mbalimbali ya sekta ya afya, elimu, maji na miundombinu ya barabara akisema wamejiandaa kuendelea kuwatumikia wananchi.
Alichokisema Kembaki, Matiko
Akizungumza baada ya uteuzi huo, Kembaki amesema ameupokea kwa mikono miwili huku akisema CCM katika Jimbo la Tarime iko mikono salama na kwamba ataitendea haki nafasi hiyo kwa kuhakikisha anatafuta kura za chama hicho kuanzia ngazi ya udiwani hadi urais.
“Hizi ni taratibu za chama chetu na ninazijua vizuri kwani hata mimi mwaka 2020 nilikuwa wa pili, lakini chama changu kiliniteua kuwa mgombea na hatimaye kuwa mbunge kwa hiyo uamuzi uliofanywa sina shida nao kwani huu ni utaratibu wa kawaida,” amesema Kembaki.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Matiko amewaondoa hofu watu wanaojiuliza kama kweli ameamua kuhamia CCM na kusema kwamba uamuzi huo ni wa uhakika na wala wasiwe na hofu.
“Ndiyo ni kweli nipo CCM kwasababu mbalimbali kubwa zaidi ni kwamba CCM ni chama chenye dira ya kuhakikisha kinaleta maendeleo kwa watanzania wote,” amesema Matiko.
Matiko amesema katika kipindi cha miaka minne iliyopita chini ya Serikali ya Awamu ya Sita, chama hicho kimefanya mambo makubwa ya kimaendeleo kwa kutekeleza miradi mingi ya maendeleo ikiwamo ukamilishaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Mwalimu Nyerere maarufu Kwangwa.
“Hospitali ya Kwangwa ilianza kuongelewa tangu Bunge la 10 lakini Serikali ya awamu ya sita ilisikia kilio chetu ikatoa mabilioni ya fedha kukamilisha ujenzi ule na na sasa tumeondokana na shida ya kwenda Bugando hivyo nimeamua kujiunga CCM kusaidia kuleta maendeleo zaidi,” amesema.
Kada wa CCM, Mchungaji Peter Msigwa amesema kuongoza nchi sio kama kuongoza sebule ya mtu binafsi na kwamba suala la uongozi linahitaji mambo mengi ikiwepo hekima,busara, ustahimilivu wa kisiasa na chama chenye sera na ilani nzuri inayotekelezeka.
Amesema sifa hizo zipo CCM chini ya mgombea urais wake Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza Dk Nchimbi na kwamba ana amini chini ya Samia na CCM nchi itakuwa salama na yenye maendeleo muda wote.
“Kuongoza nchi sio kama kuongoza sebule yako kwamba leo utaamua makochi yaangalie kushoto kesho yaangalie kulia,uongozi wa nchi unahitaji hekima busara na ustamilivu wa kisiasa na hizi sifa utazipata kwa Samia pekee,” amesema Mchungaji Msigwa, aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini kupitia Chadema.
Mchungaji Msigwa ameongeza kuwa, CCM imefanya mambo mengi mazuri na makubwa ambayo yeye na wenzake wa upinzani walikuwa wakiyapigia kelele,hivyo kutokana na utendaji kazi mzuri wa Samia hakuna sababu ya kumtafuta kiongozi mwingine zaidi ya Samia na Dk Nchimbi.
Amesema CCM ina ilani inayotekelezeka na sera nzuri, hivyo kuipa kura kwenye uchaguzi ni uamuzi wa busara kwani chama hicho kina uzoefu wa kuongoza na chini ya CCM nchi itakuwa salama.
Mwenyekiti mstaafu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma, Hamisi Alli akizingumza kwenye mkutano Rorya amesema Watanzania wanapaswa kukipigia kura Chama cha Mapinduzi, kwani ndicho kinachoaminika badala ya vyama vingine ambavyo vipo kwa ajili ya kufanya majaribio.

“Hivi unakuja kufanya majaribio kwa watu milioni 67 kweli, hii ni sawa na abiria kupanda basi linalofanya majaribio, hivi mtakuwa na uhakika wa kufika kweli, basi la uhakika lenye dereva na kondakta wa uhakika ni CCM tu,” amesema.
Amesema katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake, Samia amefanya mengi kwa faida ya Watanzania, hivyo hakuna sababu ya wao kuvipigia kura vyama vingine kwa kuvipigia kura ni kusababisha majuto katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Amesema Watanzania wanapaswa kukipima chama chake kwa yale yaliyofanyika sambamba na mipango yao ijayo.
Ameeleza kuwa, mipango ijayo inalenga kuwaletea maendeleo zaidi wananchi ili wawe na maisha bora zaidi.
“… Samia hana wa kulingana naye, kwa muda wake wa uongozi ameboresha huduma nyingi za kijamii; mfano kwenye sekta ya afya, mambo mengi yamebadilika hata upasuaji wa ubongo hivi sasa unafanyika bila mtu kupasuliwa.
“Lakini kwenye elimu ndiyo usiseme, madarasa yana vigae, vyoo vina maji na kuna umeme wa kutosha yaani mazuri ni mengi,” amesema.
Amesema saula la amani pia ni kitu muhimu ambacho Watanzania wanapaswa kuzingatia kwa maelezo kuwa, maendeleo yote yaliyofanyika yamewezekana kutokana na amani iliyopo.
Mgombea ubunge wa Rorya, Jafari Chege amesema wakazi wa Rorya hawawezi kumsahahu Samia kwa namna alivyosaidia kundokoana na changamoto ya vifo vilivyokuwa vikitikea kutokana na kusombwa na maji ya mito Mori na Wamaya inayounganisha tarafa tatu ndani ya jimbo hilo.
“Tumejengewa madaraja na vivuko sita ingawa ni midogo lakini kwa sasa watu hawapotezi maisha, watu wanavuka kwa usalama kabisa sasa hapa tutamsahau vipi mama,” amehoji Chege.
Amesema Mji wa Shirati ulikuwa ukikabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji, lakini ilipata suluhisho ndani ya siku 100 za mwanzo za Samia baada ya kumuagiza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kutatua changamoto hiyo, hivyo mji huo kwa sasa una maji ya uhakika.