Haroun Mandanda kutua Polisi Tanzania

TIMU ya maafande wa Polisi Tanzania iko katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa aliyekuwa kipa wa kikosi cha Tabora United, Haroun Mandanda baada ya kumaliza mkataba, huku kukiwa hakuna mazungumzo ya kuongeza mwingine.

Nyota huyo aliyetamba na timu mbalimbali za Mbeya City, Ihefu (Singida Black Stars) kisha baadaye pia kujiunga na Tabora United, amefikia uamuzi huo baada ya kufanya pia mazungumzo na kocha wa kikosi hicho, Mbwana Makatta.

Makatta amejiunga na Polisi akimrithi Mussa Rashid aliyetokea Biashara United aliyeiongoza kwa msimu wa 2024-25 katika Ligi ya Championship na kumaliza nafasi ya 10 kwa pointi 33 baada ya kushinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13 kati ya 30.

Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata, zinaeleza Mandanda amevutiwa na mradi wa Polisi TZ kutokana na aina ya nyota wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu wa 2025-26, jambo lililomvutia kuamua kusaini mkataba wa mwaka mmoja kikosini.

Kikosi hicho kinapambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-23, kilipomaliza katika nafasi ya 15 kwa pointi zake 25, kufuatia kushinda mechi sita, sare saba na kupoteza 17, kikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.

Polisi imesajili nyota wapya wanane wakiwamo, Ramadhan Kapera (TMA), Hamad Nassoro (KenGold), Naku James (Mbuni), Lazaro Mlingwa, Ibrahim Isihaka, Jamal Mtegeta (Pamba Jiji), Rajab Athuman (Stand United) na Joseph Majagi (Geita Gold).