Ibenge: Subirini mechi ya kwanza muone!

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge amesema timu yake bado inaendelea kujifua kwa ushindani na itakuwa tayari siku ya mechi ya kwanza ya michuano iliyo mbele yao.

Timu inatarajia kuvaana na Al Merrikh Bentiu ya Sudan Kusini katika Kombe la Shirikisho Afrika mechi ambayo imepangwa kuchezwa Septemba 19 na marudiano ni Septemba 26 katika mechi za awali za mashindano hayo ambapo itaanzia ugenini.

Kocha ameyasema hayo muda mfupi baada ya kuambulia suluhu dhidi ya Vipers katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa kwa Azam FC ambayo imeweka kambi ya kujiandaa na msimu nchini Rwanda.

Akizungumzia maandalizi hayo, Ibenge alisema timu yake inaendelea kujengeka siku hadi siku na kumpa wakati wa kubadilika kwenye mifumo ili kujenga timu bora na yenye ushindani ndani na kimataifa.

“Sio mbaya bado tunaimarika kulingana na mechi tunazocheza timu inaendelea kufanya vizuri kwa kuingia kwenye mifumo yangu wachezaji wataendelea kujifua kidogo kidogo watakuwa tayari siku ya mchezo wa kwanza,” alisema na kuongeza;

“Kwa mujibu wa mechi tulizocheza tukiwa huku tulianza mdogo mdogo sasa tunaendelea kuimarika nafikiri suala la utayari kwa wachezaji ni mapema sana kusema ila utayari utaonekana siku moja kabla ya mechi ya mashindano.”

Akizungumzia ratiba alisema ameiona na anaziheshimu timu watakazokutana nazo, lakini kwa sasa wanaendelea kujifua kwa ajili ya mashindano yote yaliyo mbele yao kwa lengo la kusuka kikosi cha ushindani.

“Ratiba nimeiona naendelea kujenga timu yangu utayari bado, mechi zote zilizo mbele yangu ni sawa. Kinachotakiwa ni utayari na ushindani jambo ambalo naamini litafanyika muda ukifika.”

Azam bado ipo nchini Rwanda na mara baada ya kurejea itakuwa na safari ya kwenda kucheza mchezo wa utambulisho wa wachezaji wa Mbeya City iliyorejea msimu huu na mchezo wao wa kwanza wa ligi ikiwa chini ya Ibenge utakuwa dhidi ya Singida Black Stars Oktoba 30.

Kikosi hicho kikiwa nchini Rwanda kimecheza mechi dhidi ya Polisi FC na kutoka sare ya bao 1-1, ikachapwa 1-0 na AS Kigali, ikashinda mabao 2-0 dhidi ya APR FC, na suluhu dhidi ya Vipers.