Jacob Massawe awatolea uvivu mawakala

KIUNGO mshambuliaji wa Namungo, Jaccob Massawe amesema mawakala wanapaswa kuacha tamaa na kuangalia malengo ya wachezaji wadogo akitolea mfano ishu ya Clement Mzize.

Mkongwe huyo anayeitumikia Namungo kwa msimu wa tano sasa tangu ajiunge nayo msimu wa 2020/21 akitokea Gwambina.

Akizungumza na Mwanaspoti, Massawe mwenye uwezo wa kucheza kama winga amesema mawakala wengi wanakwamisha viwango vya wachezaji kutokana na tamaa akitokea mfano ishu ya Mzize ambaye inadaiwa alipata ofa mbalimbali za nje, lakini Yanga ilimboreshea maslahi yake na kumbakisha.

Ameongeza wachezaji kama Mbwana Samatta anayekipiga Le Havre, Novatus Miroshi wa Goztepe na Simon Msuva ni miongoni mwa wachezaji ambao mawakala wao walikuwa vizuri katika kutafuta timu na huko wanacheza.

“Unajua ndio maana vijana wadogo wanakwenda nje wanashindwa wanarudi tena Bongo, sio wote wanashindwa kwa sababu hawawezi lakini unapeleka vipi nje?” Ameohoji Massawe na kuongeza;

“Wakala waangalie vipaji vya vijana na malengo yao mfano unampeleka Mzize au yeyote Tunisia au Libya kule atacheza michuano ya kimataifa, je kule atapata nafasi au atakwenda kurudi nyuma, nje sio pesa tu bali hata nafasi ya mchezaji ndio kitu muhimu.

“Lakini kumbe akibaki Yanga anaweza kucheza michuano ya CAF na kuisaidia timu yake pengine hata akapata dili nyingine kubwa na akacheza akaonekana.”

Massawe alianza kucheza soka la kulipwa msimu 2011 akiwa na Toto Africans, African Lyon, JKT, Ndanda FC, Stand United, Gwambina na sasa Namungo.

Licha ya kucheza kwa muda mrefu kiungo huyo hakuwahi kuichezea timu ya taifa Taifa Stars, huku akiwa bado na matarajio makubwa ya kuupiga.