Arusha. Halmashauri ya Jiji la Arusha imepanga kuanzisha Mahakama Maalumu ya Jiji, itakayoshughulikia kesi za walipa kodi na ushuru wanaokwepa au kukwamisha ukusanyaji wa mapato, ili kuharakisha uendeshaji wa mashauri na kuongeza ufanisi wa mapato ya ndani.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, John Kayombo, amesema hayo jana Jumamosi, Agosti 30, 2025, katika hafla ya kuwapongeza watumishi wa idara ya mapato waliowezesha ukusanyaji wa Sh41.3 bilioni, sawa na asilimia 90 ya makusanyo ya mwaka wa fedha 2024/2025.
Amesema halmashauri ilikadiria kukusanya Sh46.1 bilioni kupitia vyanzo vya ndani pamoja na vipya vilivyobuniwa, ikiwamo mgawanyo wa jiji katika kanda za kikodi ili kusimamia mapato kimkakati.
“Mahakama hii maalumu ya kodi na ushuru itakuwa njia rafiki na rahisi ya kushughulikia kesi kwa haraka, hivyo kupunguza changamoto za ukusanyaji mapato,” amesema Kayombo.
Ameongeza kuwa mpango wa mwaka wa fedha 2024/2025 umelenga ukusanyaji shirikishi kuanzia ngazi ya makao makuu, kanda, kata hadi mtaa, ili kuwarahisishia walipa kodi kufikia huduma hizo.
Kwa mwaka wa fedha 2023/2024, halmashauri ilikadiria kukusanya Sh48.9 bilioni lakini ilikusanya Sh35.1 bilioni pekee, sawa na asilimia 72 ya malengo.
Aidha, amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, halmashauri imejiwekea mikakati mipya ikiwamo kuimarisha kanda sita za ukusanyaji mapato kwa kutumia mifumo ya Tehama iliyoboreshwa, kuanzisha kanzidata ya wafanyabiashara, pamoja na kuongeza magari na rasilimali watu.
Katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ameipongeza menejimenti ya jiji kwa ubunifu wa ukusanyaji mapato yaliyowezesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tumefanikisha makusanyo haya kwa nidhamu ya watumishi, na tumeshuhudia fedha zikielekezwa kwenye vikundi vya wananchi kwa asilimia 10 na miradi ya maendeleo ikitekelezwa kupitia mapato ya ndani,” amesema Mkude.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa halmashauri inaweza kuongeza zaidi mapato iwapo itaimarisha usimamizi wa sheria ndogo ndogo na kuziboresha kwa kushirikisha wadau mbalimbali, wakiwemo madiwani na wanasheria.
Katika kutambua mchango wa watumishi waliowezesha makusanyo, halmashauri imewazawadia vyeti, fedha taslimu kati ya Sh400,000 hadi Sh1 milioni, pamoja na kuandaa ziara ya mafunzo kwenye halmashauri zinazokusanya mapato kwa kiwango kikubwa zaidi, zikiwamo Temeke, Kinondoni na Jiji la Dar es Salaam kuanzia Jumatatu, Septemba mosi, 2025.