USHINDI wa mabao 2-0 iliyoupata Pyramids dhidi ya Al Ahly, umetibua mambo katika klabu hiyo mabingwa wa kihistoria wa Ligi ya Mabingwa Afrika na sasa moto unawaka huku anayesakwa ni aliyeikataa Yanga.
Ni hivi. Kocha wa Al Ahly, Jose Riveiro amekalia kuti kavu ligi kuu ya Misri, akihesabu siku baada ya kuanza vibaya akiwa na kikosi hicho ambacho katika michezo minne imeshinda mmoja, sare miwili na kupoteza mmoja dhidi ya Pyramids na hivyo kumwongezea presha kocha huyo.
Kipigo hicho cha Pyramids kimeibua mazito, kocha huyo raia wa Hispania akionekana hafai kukifundisha kikosi hicho huku mastaa wa zamani wa klabu hiyo wakimsakama kutokana na mwenendo wa timu hiyo.
Kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 21 na inayoongozwa na Zamalek yenye pointi 10 ikicheza michezo minne, ikifuatiwa na Al Masry yenye nane na michezo minne na Pyramid ikiwa ya tatu na imecheza mitano na pointi zake nane, huku Al Ahly inakamata nafasi ya 12 ikiwa na pointi sita.
Katika mchezo huo ambao Ahly ilikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Al-Salam, mabao ya ushindi ya Pyramids ambayo ni mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika na inayotumikiwa na straika wa zamani wa Yanga, Fiston Mayele jana yalifungwa na mshambuliaji Walid El Karti dakika ya tano na 68.
Katika mchezo huo, Mayele ni kama alikosa bahati kwani aliwasumbua mabeki wa Ahly na shambulizi la dakika ya nne akiangushwa nje kidogo ya eneo la hatari, ndiyo lililotengeneza bao la kwanza.
Kabla kutua Al Ahly, Riveiro alikuwa katika mazungumzo ya kuja kuinoa Yanga baada ya kutangaza mapema kuachana na Orlando Pirates ya Afrika Kusini, aliyoipa nguvu kubwa, hata hivyo, alichomoa na kisha kupewa shavu kwa wababe hao wa Misri.