Kitambi aibukia Fountain Gate kumrithi Mnigeria

FOUNTAIN Gate katika kuboresha kikosi hicho kwa msimu wa 2025-2026, imemchukua Denis Kitambi kuwa kocha mkuu.

Kitambi aliyewahi kufundisha timu mbalimbali za Ligi Kuu ikiwemo Simba, Namungo, Geita Gold na Singida Black Stars, anachukua nafasi ya Mnigeria, Ortega Deniran.

Taarifa za uhakika kutoka ndani ya kambi ya Fountain Gate, zinasema uamuzi wa kumchukua Kitambi umekuja baada ya Ortega kuondoka ghafla kambini.

“Kitambi ndiye kocha wetu mkuu, ingawa bado hatujamtambulisha rasmi, uamuzi wa kumchukua umekuja baada ya Ortega kuondoka,” amesema mtoa taarifa kutoka ndani ya Fountain Gate.

Kwa mujibu wa mtoa taarifa huyo, sababu za Ortega kuondoka ghafla ni kitendo cha kupoteza mchezo wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Pamba Jiji ambao timu hiyo ililazwa mabao 2-0.

“Tulipocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga kila mmoja aliona timu ilicheza vizuri, licha ya kufungwa 2-1 lakini watu hawakusema kitu.

“Pia mchezo wa kirafiki dhidi ya Mashujaa tulipoteza kwa bao 1-0, timu ilicheza vizuri, tatizo likawa matokeo.

“Mchezo wa tatu dhidi ya Pamba Jiji tukafungwa 2-0, bosi akaona kama vile kocha ameshindwa kuiunganisha timu, akamwambia asipoifikisha fainali katika mashindano ambayo tumeyaandaa, kuna hatari ya kibarua chake kuota nyasi.

“Siku chache kabla ya kuanza mashindano tukiwa tunajiandaa kutoka Morogoro kurudi Babati, akachukua mabegi yake na kuaga anaenda kwao na uwezekano wa kurudi ni mdogo, ndio maana tumemchukua Kitambi,” amefichua mtu huyo.

Ortega alikabidhiwa kikosi cha Fountain Gate kukiongoza msimu wa 2025-2026 akichukua nafasi ya Mohamed Ismail ‘Laizer’ aliyefanikiwa kuibakisha timu hiyo Ligi Kuu Bara kupitia mechi za mtoano.

Wakati huohuo, Mwanaspoti limemshuhudia Kitambi akiwa na kikosi cha Fountain Gate ambacho jioni ya leo Agosti 31, 2025 kitacheza dhidi ya Tabora United katika mashindano maalum ya kujiandaa na msimu wa 2025-2026 yaliyoandaliwa na Fountain Gate yakifanyika keenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara.