Tumsifu Yesu kristu. Nakusalimu kwa Jina la Bwana wetu Yesu kristo aliye hai. Ninamtukuza Mungu kwa ajili yako kwa kuendelea kuachilia neema ya uhai kwako na kwa familia yako. Ni imani yangu kuwa unaendeleaa vizuri katika safari hii ya kuutafuta ufalme wa Mungu. Mungu akubariki.
Nikukaribishe kuungana nami katika tafakari ya ujumbe wa leo unaosema, ”Kujihesabia haki” Naamini ujumbe huu umekuja Mahususi kabisa kwa ajili yako na ni maombi yangu kwa Mungu kuwa ujumbe huu utafanyika uponyaji kwako lakini pia utapata nafasi ya kuweza kuwasaidia wengine.
Kujihesabia haki ni hali ya mtu kuona yuko sahihi katika maeneo yote. Mtu anaejihesabia haki hakuna mahala anahisi kupungua. Hebu soma nani maneno ya Mungu kutoka katika kitabu cha Luka:18:10-12. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; “ Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine; wanyang’anyi,wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.” Mfano huu wa Farisayo unawakilisha sote tulio na roho ya kujihesabia haki, kupiti mfano huu tunaweza kuona ni nini kinatokea pale mtu anapojihesabia haki.
Jambo la kwanza, mtu anayejihesabia haki mara zote huona makosa ya wengine. Angalia ule mstari 11, anasema “Mimi siyo kama hao…” Yaani nakwambia ukiwa karibu na mtu wa namna hii utapata tabu sana, fanya ufanyavyo bado atakukosoa, atakurekebisha, atakukemea na kutaja madhaifu yako, kwa kifupi hataona zuri kwako hata mara moja kwa sababu huamini kuwa yeye tu ndiye huwa sahihi. Mungu akuponye siku hii ya leo ili uwe wa kwanza kuondoa boriti ndani ya jicho lako ndipo uweze kukiona kibanzi ndani ya jicho la ndugu yako. Luk 6:41.
Jambo la pili, si mwepesi kuomba msamaha. Hivi inawezekana kweli kuomba msamaha wakati huoni pale umekosea? Farisayo anapoenda mbele za Mungu anatirirka tu mazuri anayoyafanya kana kwana yeye ni malaika, hakosei. Lakini ile 1Yoh 1:8 inasema “Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo mwetu” na tunamfanya Mungu kuwa muongo. Sasa ebu pata picha kama tu kanisani haombi msamaha vipi kwako anaweza kukuomba msamaha kweli? Sawa tusema alikuwa vizuri na hakuwa na kosa kabisa; Je! alifanya yote mazuri aliyotakiwa kuyatenda kwa siku hiyo sawa sawa na Yakob.4:17 Basi yeye ajuaye kutenda mema wala hayatendi, kwake huyo ni dhambi. Jambo la tatu, hakubali kushauriwa. Ukiona wewe hupendi kushauriwa basi elewa una roho ya kujihesabia haki. Tuna ndugu wengi tunafanya nao kazi, tunaabudu nao, tunashirikiana nao katika mambo mbalimbali na wengine ni viongozi wetu, lakini anapokwenda kinyume na ukaenda kwa ajili ya kumshauri hapo uwe umejipanga na ni huruma kwao kwa sababu, sababu ya jeuri zao tumewaacha wafanye watakavyo lakini mwisho huwa wanaweza kujikuta wako peke yao na wengine tunaishi nao ili tu siku ziende na maisha mengine yaendelee ili kuepuka shari zao. Mungu akuponye, nyenyekea acha ubabe hakuna aliyemkamilifu.
Jambo la nne, mtu anayejihesabia haki amejaa majivuno. Mfano mzuri wa Farisayo anapokuwa mbele za Mungu anasema “mimi si kama kama watu wengine…” Farisayo alijivunia utajiri wake na hadhi na anapojifananisha na Mtoza uhuru anaona kabisa hawaendani, majivuno huamabatana na dharau kuwaona wengine si kitu na kujiona wewe ni bora zaidi yao. Je hali hii ya ajivuno imo ndani yako? Unawachukuliaje watu wa hali ya chini au walioanguka katika dhambi? Unawaona hawafai mbele za Mungu? Wacha nikwambie kitu wenye afya hawana haja na tabibu,isipokuwa waliohawawezi. Luka 5:31. Ukiona kwamba umejikamilisha ni wasa, lakini acha kudharau wengine.
Unaweza fanya yote mazuri lakini kama ni mtu wa kujihesabia haki yote unayoyafanya ni bure. Pamoja na Farisayo kutoa zaka na kujisifia kote alikofanya lakini aliye hesabiwa haki ni mtoza ushuru kwa sababu yeye alipofika mbele za Mungu alisimama mbali ,wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipigapiga kifua akisema, Ee Mungu uniwie radhi mimi mwenye dhambi.
Pata nafasi siku ya leo ya kwenda mbele za Mungu kwa unyenyekevu na kuomba toba, mwambe Mungu akusamehe kwa uovu wote ulioutenda, yamkini wengi tuko na tabia kama za Farisayo, tunapoenda mbele za Mungu nasi husema Mungu mimi si kama mama fulani au familia ya fulani, natoa michango mingi kanisani, kitu hiki na kile pale kanisani ni mimi nimetoa na leo nimemnunulia suti mchungaji.
Ndugu yangu sifa hizi zote hazihitajiki, unapotoa toa kama kwa Bwana na wala usitamani kila mtu ajue. Yeye aonaye siri atakujazi. Mungu akubariki sana, nikutakie Baraka za Bwana wewe na familia yako. Usichoke kuutafuta uso wa Bwana. Mtafue maadamu anapatikana, mwite naye atakuitikia. Shalom.
Mwalimu. Peace Marino, Anapatikana Usharika wa KKKT Ebeneza Nyashimo, Busega. Kwa maombi na ushauri. 0783999044.