Lindi. Mkoa wa Lindi umeweka dhamira ya kuhakikisha vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga vinapungua hadi kufikia tarakimu moja.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili, Agosti 31, 2025 na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Kheri Kagya katika kikao kazi cha siku tatu cha kujadili vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga ngazi ya mkoa, kilichokutanisha timu za wasimamizi wa afya ngazi ya halmashauri na mkoa (CHMT na RHMT).
“Tuna kila sababu ya kujivunia mafanikio tunayoendelea kuyapata katika mapambano dhidi ya vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga. Mafanikio haya yametokana na uwajibikaji wa uongozi na watendaji katika sekta ya afya. Takwimu zinaonesha kuwa kuanzia Januari hadi Juni 2025, tumeshuhudia vifo tisa pekee mkoa mzima,” amesema Dk Kagya.
Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uzalishaji na Rasilimali Watu, Nathalis Linuma amesema tathmini inaonesha ongezeko la kinamama wanaojifungua katika vituo vya afya kutoka asilimia 96 mwaka 2021 hadi asilimia 98 mwaka 2024.
Amesema ongezeko hilo ni ishara nzuri, huku akisisitiza wataalamu wa afya kuboresha huduma bora kwa mama na mtoto.
Linuma amewataka wataalamu kuhakikisha wajawazito wanapata elimu ya umuhimu wa kuhudhuria kliniki katika miezi ya awali ya ujauzito, ili kufikia lengo la Serikali la asilimia 60.

Amesisitiza pia, kuimarisha matumizi ya watoa huduma ngazi ya jamii (CHW) katika kuelimisha na kushawishi wananchi kuhusu umuhimu wa huduma za awali kwa wajawazito.
“Niwaombe wataalamu wa afya kujitahidi kutoa huduma bora kwa mama na mtoto, ili tuweze kufikia lengo la Serikali la kupunguza vifo kwa asilimia 60,” amesema Linuma.
Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Kanda ya Kusini, Sophia Mchinjita ameipongeza Lindi kwa uratibu mzuri wa uchangiaji na ukusanyaji wa damu salama.
Amesema mwaka 2024, mkoa huo umeongoza kitaifa kwa kampeni ya uchangiaji damu, hatua iliyosaidia kuokoa maisha ya mama wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua na watoto wachanga wenye changamoto hiyo.
“Damu zinazochangiwa zinatumika kama akiba ya dharura. Zinaokoa maisha ya wakinamama na watoto wachanga wanaohitaji msaada huo,” amesema Mchinjita.
Vilevile, ameipongeza Halmashauri ya Kilwa kwa mafanikio makubwa ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi.
Amesema mwaka huu Kilwa imeripoti kifo kimoja pekee, ikilinganishwa na miaka ya nyuma ilikuwa kinara kwa kuwa na vifo vingi.