Mahakama yaamuru KKKT Konde kulipa Sh133.5 milioni michango ya wafanyakazi NSSF

Arusha. Mahakama Kuu Masijala Ndogo ya Mbeya imeiamuru Bodi ya Wadhamini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Konde, kulipa michango ya wafanyakazi wake kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), zaidi ya Sh133.5 milioni.

Fedha hizo ni malimbikizo ya michango ya wafanyakazi wa Shule ya Manow Lutheran Junior Seminary, ambao ni wanachama wa NSSF kwa kipindi cha Novemba 2018, Januari 2019 hadi Desemba 2022.

Maombi hayo ya madai namba 21/2023 yalifunguliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Bodi ya Wadhamini wa NSSF, wakidai Bodi ya Wadhamini KKKT Dayosisi ya Konde kushindwa kutuma michango ya wanachama.

Kutokana na hali hiyo, wadai hao wawili walidai zaidi ya Sh235.3 milioni ikiwa ni michango ya wanachama ambayo haijarejeshwa pamoja na faini zinazopaswa kulipwa.

Hukumu hiyo imetolewa Agosti 29, 2025, na Jaji Musa Pomo, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, ambapo baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili na kupitia vielelezo vilivyowasilishwa mahakamani, aliamuru Bodi ya Wadhamini KKKT Dayosisi ya Konde kulipa Sh133.5 milioni ya malimbikizo ya michango ya wafanyakazi wake.

Ilidaiwa mahakamani kuwa mdaiwa ameshindwa kupeleka michango ya wanachama NSSF kwa baadhi ya miezi, yenye thamani ya zaidi ya Sh133.5 milioni kati ya kipindi kilichotajwa, na adhabu ya kulimbikiza Sh101.8 milioni, kufanya jumla iwe zaidi ya Sh235.7 milioni.

Julai 16, 2025, wakati shauri hilo lilipotajwa kwa ajili ya usikilizwaji, upande wa AG na NSSF waliwakilishwa na Wakili wa Serikali, Michael Fyumagwa, huku dayosisi hiyo ikiwakilishwa na wakili Peter Kiranga.

Katika kuunga mkono kesi yao, wadai walikuwa na shahidi mmoja, Mvumo Hassan, ambaye pia alitoa vielelezo saba, huku mdaiwa akiwa na shahidi mmoja, Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Konde, Benjamin Mbembela.

Mvumo, Ofisa Matekelezo wa NSSF, alieleza mahakama kuwa miongoni mwa majukumu yake ni ufuatiliaji wa utumaji wa michango ya wanachama kwenye mfuko huo.

Alieleza kuwa anamfahamu mdaiwa katika nafasi yake kama mwajiri mchangiaji, akiwa mmiliki wa shule hiyo, na kudai kuwa kwa kipindi cha Novemba 2018, Januari 2019 hadi Desemba 2022, mshtakiwa alishindwa kupeleka michango ya watumishi hao kwa NSSF.

Kutokana na makosa hayo, hatua mbalimbali zilichukuliwa kujaribu kuhakikisha mshtakiwa anatimiza wajibu wake, lakini jitihada hizo zilionekana kuwa bure.

Aidha, Mvumo alitoa nyaraka kadhaa ikiwemo notisi ya ukaguzi wa kisheria, ratiba ya malimbikizo ya michango ya kisheria, notisi ya kulipa siku saba, notisi ya malipo ya kuchelewa, na notisi ya adhabu, ambapo alihitimisha ushahidi wake kwa kueleza kuwa hadi sasa wanadai zaidi ya Sh235.3 milioni.

Katika utetezi wake, Katibu Mkuu wa Dayosisi hiyo alisema kuwa anakaimu kama mwajiri kwa niaba ya kanisa na ndiye mlinzi wa nyaraka zake zote rasmi. Aidha, alidai hatambui kiasi kinachodaiwa na walalamikiwa, hasa Sh133.5 milioni, kwa maelezo kwamba utaratibu uliowekwa wa tathmini ya madai hayo haukuzingatiwa na kuwa baadhi ya vielelezo havikuwa vya kweli na havikuonesha kwa usahihi hali halisi ya madai yaliyodaiwa dhidi ya mshtakiwa.

Jaji Pomo amesema amezingatia kwa makini ushahidi uliotolewa pamoja na pande zote mbili na kwamba ataangalia suala la kwanza la kuamua, ambalo ni kuhusu michango pamoja na adhabu.

Amesema majukumu ya kiutawala ya shule, kama yalivyoelezwa, ni ya mshtakiwa, ambaye ana wajibu wa kufuatilia na kuhakikisha uzingatiaji wa masuala yote yanayohusu shule, ikiwa ni pamoja na kupeleka michango ya wafanyakazi kwa NSSF.

Jaji Pomo amesema anaona wadai wamefaulu kuthibitisha kuwa mshtakiwa alishindwa kutimiza wajibu wake wa kisheria wa kupeleka michango ya wafanyakazi NSSF, kama ilivyothibitishwa na vielelezo kadhaa.

“Nimeridhika kwamba walalamikaji walithibitisha madai yao, japo kwa kiasi fulani, na naamuru mshtakiwa kuwalipa walalamikaji Sh233.5 milioni ikiwa ni michango ya wanachama kati ya Novemba 2018, Januari 2019 hadi Desemba 2022, na gharama za shauri zitalipwa na mshtakiwa,” amesema Jaji Pomo.