Dar es Salaam. Inawezekana ukaishi na watoto au mtoto wako nyumbani lakini akahisi kama vile haupo.
Labda kwa lugha nyingine naweza kusema unaweza kuwepo nyumbani kimwili “physically” lakini usiwepo kihisia na kijamii “absent socially and emotionally” na hapa ndipo wazazi na walezi wengi tulipo pasipo kujua na huku tukidhani kuwa mambo yote baina yetu na watoto wetu yako sawa.
Ukweli ni kwamba hali sio shwari hata kidogo na kwa bahati mbaya, mbegu hii mbovu inayopandwa wakati huu inaota na kumea na kuleta uharibifu wa kudumu katika maisha yote ya mwanao au wanao. Nakushauri ujifunze kubadilika.
Hapa nina vitu vichache ambavyo ni mifano tu ya jinsi au namna ya kukuza na kuendeleza ukaribu au uhusiano baina ya wewe mzazi na mtoto wako.
Nina watoto wawili wa kike lakini nyumbani kwangu huwa kuna watoto zaidi ya wawili mara nyingi.
Hii ni kwa sababu watoto hawa kutoka nyumba za jirani wamejenga uhusiano mzuri wa mzazi na mtoto na mimi kuliko walivyojenga na wazazi wao.
Kwa hiyo kwao kukaa nyumbani kwangu, wakila, kunywa na kufurahia urafiki na hali ya wao kuwa katika “familia” kunawafanya washinde kwengine mchana na kwenda kulala kwingine usiku.
Unaweza kutengeza mazingira ya wanao kuwa na uhusiano bora baina ya mzazi na mtoto. Kuna vitu vichache vya kuzingatia;
Moja, waonyeshe na kuwahakikishia upendo wa kweli. Wasaidie kupunguza au kuondoa hofu wanapokuwa na wewe au kuongea na wewe. Watoto wako wanatakiwa wakuheshimu kwa upendo sio kukuogopa.
Mbili, furaha na upendo wako kwao uwe wa wakati wote, usiwe wa msimu au baadhi ya vipindi.
Ukaribu baina yako na wao uwe wa asubuhi ukitoka kwenda kazini au wao wakitoka kwenda shule na hata wanapoimaliza siku yao wakienda kitandani.
Ruhusu wakuone na kuhisi uwepo na upendo wako katika ndoto zao. Hii ni pamoja na kuongea nao matarajio yao maishani pamoja na kusoma nao hadithi wakiwa kitandani.
Ninapozungumzia kuwa nao kihisia na kijamii ninamaanisha kuwaruhusu kukugusa, kucheza na wewe, wao kufahamu hisia zako na wewe kufahamu hisia zao.
Wakati wote ukiwa nao wahisi mguso wa kihisia wa kipekee kabisa tofauti na wanapokuwa na mwalimu wao au mtu mwingine hapo nyumbani.
Tatu, wakati unawahimiza kuhusu maisha yao ya baadaye na umuhimu wa kusoma na kujifunza ili kuwa na kesho njema, hakikisha hauongei maneno tu bali unakuwa nao katika mchakato.
Waruhusu kukuuliza swali pale wanapohitaji msaada, pata muda hata kama ni mara chache kukaa nao na kushika vitabu vyao vya shule na kuwaelekeza au kusoma nao. Waruhusu wafuate nyayo zako kwa vitendo sio kwa maneno “Be their model”
Nne, pamoja na kwamba kuna usafiri wa shule unaowachukua wanao au mwanao kumpeleka na kumrudisha kutoka shule, mara moja moja pata nafasi ya kumwambia “nitakupeleka/ tutakupeleka wenyewe leo, au nitakuchukua mwenyewe.
Ukipata nafasi hii, ongea naye mambo mbali mbali ya shule, walimu wake, marafiki zake, umuhimu wa kuwa na marafiki wazuri n.k. Unaweza kujifunza mengi sana kutoka kwa mwanao mnapokuwa wenyewe kwenye gari kwa umbali wa kutoka nyumbani hadi shuleni, vitu ambavyo ungekaa miaka hujavigundua kwa kutoka asubuhi na kurudi majogoo.
Tano, mara wanapoona wana uhakika wa maisha, furaha na ulinzi, ni rahisi kuyaweka mawazo yao katika yale wanayotamani kuyafanya ikiwemo kazi zao za shule na hivyo kufanya vema darasani na maishani kwa ujumla
Ni ukweli usiopingika kwamba hata kama unatamani vipi kuwa na ukaribu sana na wanao, pale wanapokuwa wengi kiidadi katika familia, mchakato huu huathirika na hivyo athari nyingi kuwa hasi.
Tuwaruhusu watoto wetu kufurahia uwepo wetu tukiwa hai, ndiyo zawadi pekee kuliko pesa, nyumba, mashamba na magari tunayoweza kuwaachia tukifariki.
Let’s have a positive legacy: Your child, your legacy.