Mbwana Samatta mdogo mdogo Ligue 1

NAHODHA wa timu ya taifa, Taifa Stars, Mbwana Samatta ameendelea kuizoea Ligi Kuu ya Ufaransa, baada ya usiku timu anayoichezea ya Le Havre kupata ushindi wa kwanza wa mabao 3-1 dhidi ya Nice.

Katika mechi hiyo ya Ligue 1, nyota huyo wa kimataifa wa Tanzania alitumika kwa dakika 85, wakati timu ikiwa tayari inaongoza kwa mabao 2-1 akimpisha Simon Ebonog.

Samatta aliyetua katika timu hiyo hivi karibuni baada ya kumaliza mkataba aliokuwa nao PAOK ya Ugiriki, hii ni mechi ya tatu kwake, akianza dhidi ya Monaco akitumika kwa dakika 32 kisha kucheza kwa dakika 72 dhidi ya Lens na zote timu hiyo ikipoteza 3-1 na 2-1 mtawalia.

Katika mechi ya leo iliyopigwa kwenye Uwanja wa nyumbani wa Le Havre wa Oceane , mabao ya wenyeji yalifungwa na Fode Doucoure  katika ya 13, Rassoul Ndiaye aliyetupia dakika ya 61 kabla ya Issa Soumare kufunga hesabu dakika za majeruhi.
Bao la kufutia machozi la Nice lilifungwa na  Kojo Peprah dakika ya 52, likiwa ni la kusawazisha mara baada ya kuanza kipindi cha pili.